
Habari za leo mpenzi msomaji wa Mwanaharakati mzalendo naamini unaendelea vizuri na mapumziko ya sikukuu ya Pasaka. Karibu tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto kwa sababu elimu na maarifa havina sikukuu. Matatizo na changamoto havijui siku ya sikukuu, vinapokuandama vinakuandama kweli na hivyo unahitaji kuendelea kupata maarifa kila siku na kila wakati.
Katika makala ya leo tutaangalia ni wapi ambapo fedha zako zinapotea bila ya wewe mwenyewe kujua. Lakini kabla ya kufika huko tuangalie kwanza kwa nini fedha ina changamoto sana. Katika vitu vyote tunavyoweza kumiliki binadamu, fedha ndio ina changamoto kuliko vingine vyote.
Tunaona watu wengi wakifanya mambo ya ajabu sana kwa sababu ya fedha. Watu wanadanganya kwa sababu ya fedha na hata wengine wapo tayari kutoa uhai wa wenzao kwa sababu tu ya fedha.
SOMA; Tabia Hizi Zitakusaidia Sana Kufikia Malengo Yako Kwa Haraka – 2
Sehemu kubwa ya changamoto na matatizo haya ya kifedha inatokana na tabia zetu kuhusiana na fedha. Na sehemu kubwa ya tabia hizi tumejikuta tunaiga tu kutoka kwa wanaotuzunguka. Hakuna sehemu sahihi ambapo tumewahi kupata elimu sahihi ya fedha. Na kama mtu sio mpenzi wa kujifunza vitu mwenyewe kwa kujisomea, basi mtu anakwenda kwenye maisha yake yote akiwa na elimu ya kuiga kwenye matumizi ya fedha.
Changamoto kubwa ya elimu hii ya kuiga ni kwamba wale ambao unaiga kwao nao waliiga na hao pia waliiga na inakwenda hivyo mpaka zamani kabisa.
Unafikiri ni kitu gani kizuri unaweza kujifunza kwa mtu ambaye hajawahi kupata elimu sahihi ya matumizi ya fedha? Hakika utajifunza matumizi ya hovyo ya fedha.
Hivi ndivyo jamii zetu zinavyoishi hasa katika eneo la fedha. Tunatumia fedha kama kila mtu kwneye jamii yetu anavyotumia, Mwishowe tunajikuta wote kwenye matatizo ya fedha na tusijue fedha zetu zinakwenda wapi. Na uzuri ni kwmaba pale ambapo tunakuwa na matumizi mabaya ya fedha na tukashindwa kujua fedha zetu zinapotelea wapi tunayo sababu mija ya uhakika. Sababu hiyo ni CHUMA ULETE, pale tunaposhundwa kujua fedha zetu tumezitumiaje au tumezipotezea wapi, moja kwa moja tunasema chuma ulete aamechukua fedha zetu.
SOMA; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo – 2
Je unafikiri ni kweli kuna chuma ulete? Natamani ningekuambia ndio, ila ukweli ni kwamba, hakuna chuma ulete mwingine zaidi yako wewe mwenyewe. Wewe ndio unachuma fedha na kuzipeleka kwenye matumizi ambayo sio ya msingi kwako.
Sasa unawez akufanya nini ili kuondokana na changamoto hii ya kutokujua fedha zako zinapotelea wapi?
Kabla ya kuangalia ni kitu gani unaweza kufanya, kwanza tupate maoni ya msomaji mwenzetu;
mimi kitu kinacho nisumbua hela napata lakini sielewi hii hela inaishaje nikiangalia sina matumizi makubwa nilikuwa naomba unisaidia niweze kutunza hela yangu
Kama tunavyoona kwa msomaji mwenzetu hapo juu, kuna watu wengi ambao hela wanapata lakini hawajui inaishia wapi. Na wenyewe watakuambia kwamba hawana matumizi makubwa.
Matatizo yote ya fedha yanaanzia sehemu mbili tu. Sehemu ya kwanza ni kipato, yaani ni kiasi gani unapata kwenye kazi au biashara unayofanya na sehemu ya pili ni kwenye matumizi. Msomaji mwenzetu hapa amesema kipato sio shida na pia anasema matumizi sio makubwa, lakini lazima kuna kitu kimoja kati ya hivyo ambacho yeye hakijui vizuri. Kwa upande wa kipato kila mtu anajua, ndio maana watu hushawishi walipwe kiasi kikubwa. Ila upande wa matumizi hapa wengi hawajui na ndio maana mtu atakuambia sina matumizi makubwa.
SOMA; BIASHARA LEO; Kwa Nini Watu Hawawaambii Wengine Kuhusu Biashara Yako.
Mara nyingi watu hufikiri matumizi makubwa ya fedha ni mpaka unaponunua gari au kitu cha thamani kubwa. Bia moja moja ambayo mtu anakunywa karibu kila siku hahesabu wkamba ni matumizi makubwa ya fedha. Nguo ambazo mtu ananunua mara kwa mara kwa sababu ameziona hahesabu ni matumizi makubwa. Kupendelea kula vyakula ambavyo vina bei kubwa kidogo ili hali havina thamani kwenye mwili hahesabu kwmaba ni matumizi makubwa. Na hii ndio sababu watu wanapoteza fedha kila siku na wanabaki na mshangao kwa sababu vitu vingi vidogo vidogo wanavyofanya hawavihesabu.
Leo nataka nikuambie kwamba fedha zako zinapotelea kwenye hayo matumizi madogo madogo, kununua bia, soda, nguo, vyakula vya hovyo, kutoa ofa na matumizi mengine mengi madogo madogo. Unapotoa elfu moja amu tano unaweza kuona ni ndogo, ila unapokusanya fedha zote hizi kwa mwezi ni kiasi kikubwa sana.
Sasa ufanyeje?
Kwa kuwa tayari upo kwenye tatizo la fedha na umeomba msaada basi fanya mambo haya sita ninayokushauri hapa. Yafanye yote bila ya kuruka hata moja na utaona mabadiliko makubwa kwenye fedha zako. Ukishindwa kufanya utaendelea na matatizo uliyonayo sasa na maisha yako yataendelea kuwa magumu.
1. Nunua kijitabu kidogo ambacho utakuwa unaandika mambo yako yote ya fedha. Katika kitabu hiki anza kw akuandika matumizi ambayo ni muhimu sana kwako. Haya ni yale matumizi ambayo ukiyakosa unaweza kupoteza uhai wako. Hivyo chakula, chakula hasa, kinaingia, malazi, usafiri na vingine muhimu. Vitu vyote vya starehe au anasa sio muhimu sana, Kunywa soda sio muhimu kabisa, kunywa bia sio muhimu kabisa. Naamini mpaka sasa una nguzo za kukutosha kuvaa hivyo kununua nguo miezi sita ijayo sio muhimu kabisa. Fanya hivi ili uanze kuweka kipaumbele kwenye matumizi yako ya fedha.
SOMA; UKURASA WA 94; Unajiambia Nini Unapoongea Na Wewe?
2. Kuanzia leo anza kuandika matumizi yako yote ya fedha. Hata kama utatumia fedha ndogo kiasi gani iandike kwenye kijitabu chako hiki. Andika kila siku na sio usubiri mwisho wa wiki. Zoezi hili litakuchukua kama dakika tano tu kwa siku. Lakini litakusaidia sana kuanza kupata picha ya wapi fedha zako zinapotelea.
3. Anza kujilipa wewe kwanza. Katika kipato chochote ambacho utapokea, kabla hujaweka matumizi yoyote, toa asilimia kumi na weka pembeni. Iweke fedha hii mahali ambapo huwezi kuitoa kabisa. Endelea na tabia hii na ongeza kiwango kadiri siku zinavyokwenda.
4. Futa kabisa matumizi yoyote ambayo sio ya msingi wkenye maisha yako, angalau kwa kipindi hiki ambacho unataka kuondokana na tabia hii.
5. Kabla hujafanya matumizi ya fedha jipe muda wa kufikiri kama kweli maamuzi unayofanya ni sahihi. Kwa mfano kabla hujashawishika kutoa fedha zako na kununua nguo, fikiria ni nguo ngapi ambazo unazo na huwa huzivai. Hii itakuwezesha kuacha kununua vitu kwa hisia na baadae kujutia kwamba umepoteza fedha.
6. Soma kitabu KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIO TAJIRI kitabu hiki kina mambo yote muhimu unayotakiw akujua kuhusu fedha. Kukipata soma maandishi hayo ya jina la kitabu.
Fanya mambo hayo sita na zingatia yote tuliyojadili hapo juu. Elimu muhimu kuhusu fedha ndio silaha pekee itakayokuwezesha kuondokana na changamoto hii. Hapa umepata sehemu ndogo sana ya elimu hii, unahitaji kuendele akuipata kila siku, kwa sababu sio kitu rahisi. Jiunge naKISIMA CHA MAARIFA ambapo utapata elimu hii kiundani na hatua kwa hatua. Kama hutaona umuhimu wa elimu na maarifa haya hasa kuhusu fedha utaendelea kubaki hapo ulipo na changamoto zitaendelea kukuandama kwa sababu wewe mwenyewe ndio CHUMA ULETE wa fedha zako.
Maisha ni yako na ushaguzi ni wako, chagua leo kuacha kutumia fedha hovyo na chagua kuendele akupata elimu na maarifa yatakayokuwezesha kuboresha maisha yako.
Nakutakia kila la kheri.
TUPO PAMOJA.
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz |