Mwanaharakati Mzalendo

Asasi za Kiraia zaupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, zadai umelenga kuua Demokrasia nchini


Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze akizungumza wakati wa Mkutano wa asasi za kiraia kujadili juu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo asasi sita zimeupinga muswada huo.

 Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe (wa pili kulia) na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Fatma Karume wakizungumza na waandishi wa habari juu ya maoni ya asasi za kiraia juu ya Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Taasisi
sita za kiraia zikiongozwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) zimetoa
msimamo wao kuhusu Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa unaotarajiwa
kuwasilishwa Bungeni  huku wakisema endapo utapitishwa utaua demokrasia nchini.

Taasisi
hizo ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Taasisi ya
Twaweza,Baraza la Habari (MCT), Center for Strategic Litigation, pamoja na
Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza) ambazo kwa pamoja zimedai
kuwa muswada huo si rafiki katika uendeshaji wa shughuli za kisiasa nchini.

Akizungumza leo wakati wa Mkutano na waandishi wa habari,
Rais wa TLS Fatma Karume amesema endapo muswada huo utapitishwa hakuna
aatakayekuwa salama hata wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mwanasheria huyo amesema muswada huo unakwenda kinyumne na
matakwa ya Katiba inayotoa uhuru wa kijieleza na zaidi utaminya uhuru wa
kushiriki kwenye shughuli za kisiasa ikiwamo zile za utoaji wa elimu ya uraia.

“Tangu lini tunaifanya elimu kosa la jinai? ina maana
tunataka ni elimu gani mwananchi apate, hili ni jambo la kustaajabisha
sana,” alisema Karume.

Aliongeza, “Kitu nataka kuwaambia wana CCM wanadhani
kwamba wapo protected (wanalindwa) hawapo protected kabisa kwasababu sheria ni
msumeno inakata pamde zote,”.
Hatahivyo,
Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi Humphrey
Polepole, kimeunga mkono muswada huo na kwamba utasaidia kuleta uwazi na
uwajibikaji kutokana na sheria iliyopo sasa kutoakisi mazingira ya sasa.

Polepole
alisema si kweli kwamba sheria inampa madaraka makubwa Msajili wa Vyama huku
akisema muswada utasaidia kujenga mfumo thabiti wa siasa ndani ya vyama.

Mkurugenzi
wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema muswada unampa mamlaka makubwa  Msajili waVyama ambaye amemfananisha kama refa
wa mpira wa miguu ambaye ni shabiki wa timu inayoshindana.

“Refa ameajiriwa na timu moja inayoshiriki
mashindano hivyo inakuwa ngumu kutenda haki katika kipindi chote cha mchezo,mshahara
wake unalipwa na moja ya timu na timu hiyohiyo inaweza kumwondoa madarakani
kama haijaridhishwa na utendaji wake” alisema.

Wakili
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe alisema pamoja
na kuwa muswada huo una mazuri machache ikiwamo kuongeza uwajibikaji na uwazi
katika matumizi ya fedha za ruzuku, umegubikwa na mabaya ambayo yata athiri kwa
kiasi kikubwa shughuli za siasa.

Massawe
amesema endapo muswada utapitishwa, bado kuna nafasi ya kudai mabadiliko ya
sheria au kupeleka pingamizi mahakamani.

Mapungufu
yanayotajwa na asasi hizo ni pamoja na mamlaka makubwa ya Msajili wa vyama,
kuminya uhuru wa kujieleza, adhabu kali kwa makosa ya kiutendaji, kutokuwapo
kwa ujumuishwaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *