Mwanaharakati Mzalendo

Halmashauri ya Mji wa Kondoa imepongezwa kwa ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2018/2019


 

Na: Sekela Mwasubila


Afisa Habari 


Kondoa Mji


Halmashauri ya Mji wa
Kondoa imepongezwa kwa ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha robo ya pili
kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na kufikia asilimia 67 ya lengo la mwaka
na kuwa halmashauri ya 3 kwa halmashauri za miji
nchini.


Pongezi hizo zilitolewa
na Bwana Peter Gujenji kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
wakati wa kikao cha baraza la madiwani lililofanyika katika ukumbi wa
Kondoa Irangi hivi karibuni.


Alisema kuwa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa inatambua na inathamini juhudi zinazofanywa katika
ukusanyaji wa mapato na inawapongeza sana kwa juhudi hizo na inandaa
barua ya pongezi kulithibitisha hilo.


“Mwaka jana hadi robo ya
pili inaisha halmashauri ya Mji ilikusanya milioni 200 sawa na asilimia
23 ya makisio ya bajeti ya mwaka 2017/2018 lakini kwa  kipindi cha mwaka
wa fedha 2018/2019 hadi robo ya pili inaisha
halmashauri imekusanya zaidi ya shilingi 500 sawa na asilimia 67 kwa
kweli mnastahili pongezi.” Alisisitiza Bwana Peter.


Aliongeza kwa kuwasihi
viongozi wa halmashauri kuendelea kubuni mbinu zaidi za ukusanyaji wa
mapato na kuongeza uwajibikaji na upendo ili kufikia malengo
yaliyowekwa.


Akiongea katika kikao
hicho Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mhe. Hamza Mafita alisema kuwa
mapato yameongezeka baada ya kupata Mkurugenzi mpya  ambaye amewezesha
kufikia hapo na hiyo imetokana na kufanya kazi
kwa ushirikiano kati ya madiwani na menejimenti.


“Tumeongeza mashine za
kukusanyia mapato hadi kufikia mashine 25 ambazo zimegawanywa katika
kata mbalimbali kwa ajili ya kukusanya mapato na tuna mpango wa
kufikisha mashine 50 ili kuhakikisha maeneo yote yenye
mapato yanakusanywa.”Alisema Mhe. Hamza


Akielezea siri ya
ukusanyaji wa mapato Mkurugenzi wa Mji wa Kondoa Msoleni Dakawa amesema
mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo kati ya watendaji na
mikakati iliyowekwa katika ukusanyaji wa mapato.


“Tumeunda timu mbalimbali
za ukusanyaji wa mapato kwa kuweka mameneja ambapo kuna meneja wa POS,
masoko na mageti ya mazao pamoja na hizo timu pia tumetenga siku maalum
ya ukusanyaji wa mapato ambayo wakuu wa idara
hujigawa na wasaidizi wao na kwenda kukusanya mapato.”Alisema Dakawa.


Hatahivyo alitoa wito kwa
wafanyabiashara kuendelea kutoa kodi kwani wakifanikisha hilo
watawezesha halmashauri kujiendesha yenyewe lakini pia itasaidia
serikali kupata mapato na kujiendesha yenyewe bila kutegemea
misaada kutoka kwa wafadhili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *