Mwanaharakati Mzalendo

ZAHERA KIBOKO AKUTANA NA YONDANI, ATOA MPYA


Kocha huyo mwenye uraia wa DR Congo na Ufaransa, alisema kwamba wakati anaanza kukinoa kikosi hicho alionekana kugombana na Ajibu juu ya nidhamu lakini amejirekebisha kwa kiasi kikubwa na sasa ni mfano wa kuigwa.

Yondani awali alikuwa nahodha msaidizi lakini baada ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kustaafu akawa nahodha mkuu akisaidiwa na Juma Abdul ambaye ni swahiba wake mkubwa.

“Nimesikia watu wengi wakisema juu ya uamuzi wangu wa kumuondoa Yondani katika nafasi hii, naomba tu watu wote wajue kuwa sijakurupuka kufanya hivi kwani hata Yondani mwenyewe anajua kuwa kulikuwa na siku ningekuja kuchukua tu uamuzi kama huu kwani nilishamwambia abadilike lakini hakutaka kufuata maagizo yangu kwa wakati.


“Yondani amekuwa nahodha pamoja na Juma Abdul, lakini kwa nini sigombani na Juma nagombana na yeye tu, inabidi watu wafahamu kuwa siwezi kuwa na kiongozi ambaye yeye ndiye anaonekana chanzo cha kuwafanya wengine nao wakose nidhamu.

“Yondani amekuwa akifanya makosa kama haya ninamvumilia sana lakini kwa sasa nimeona bora nimpatie Ajibu ambaye atakuwa mfano kwa wengine,”alisisitiza Zahera ambaye staili yake ya kuamua kuendelea na matizi na kikosi cha kwanza Jijini Dar es Salaam imeonekana kuwatia wasiwasi Simba kutokana na ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu Bara ambayo Yanga ni vinara wakiwa na pointi 50.

“Nimeamua kumpatia Ajibu kwa sababu mwanzo alikuwa ni mchezaji asiyejitambua katika nidhamu yake na tuligombana sana kadri siku zilivyoenda alinielewa na amebalika.

“Nimempatia jukumu hili, ili awaongoze wenzake na wajue tu kuwa mtu ukiwa na tatizo halafu ukalirekebisha lazima thamani yako ipande na inaweza kuwa moja ya hamasa kwa wengine,”alisema Zahera ambaye anaishi karibu na ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam.

“Najua wengi wanajiuliza kwa nini sijampatia Juma hili jukumu na alikuwa nahodha msaidizi, ni kweli nilipaswa kumpandisha Juma ambaye ni kiongozi mwenye nidhamu na anasikilizwa na wenzake kwa kila kitu, lakini nimempa Ajibu iwe kama moja ya kuthamini mabadiliko,”aliongeza Zahera ambaye familia yake inaishi Ufaransa

“Kila mmoja alidhani Ajibu hawezi kubadilika wala kutokea siku moja akaja kuwa kiongozi wa wenzake.

“Nachukua fursa hii kuwaomba mashabiki na uongozi wa Yanga wawasapoti tu Ajibu na Juma kwa sababu sitabadilisha uamuzi wangu maana kama ni suala la kuongoza nina imani Juma atamsaidia Ajibu kwa hali na mali ili wafanikishe kutimiza majukumu ya uwanjani na nje ya timu.

“Ajibu atakuwa nahodha mkuu akisaidiwa na Juma ambaye ni mzoefu na mchapakazi ili aweze kuvuna faida ya mabadiliko ya nidhamu yake,” alisema Zahera ambaye ni Kocha msaidizi wa timu ya Taifa ya DR Congo.

Yondani kwa upande wake aliomba radhi kwa kilichotokea kwa maelezo kwamba hakufanya makusudi, alikuwa na matatizo binafsi ambayo atamueleza bosi wake ambaye ni Kocha.

VIONGOZI

HABARI za ndani zinadai baadhi ya wachezaji hawaungi mkono msimamo wa Kocha kuhusu Yondani lakini hata baadhi ya viongozi wanamshawishi Kocha abadili maamuzi.

“Wanaounga mkono wanadai kuwa kocha kafanya jambo sahihi kwa sababu Yondani kama kiongozi wa wenzake alitakiwa kuwa mfano na siyo chanzo cha utovu wa nidhamu.

“Wale wanaopinga wanadai kuwa kocha hakupaswa kufanya hivyo alipaswa kumsikiliza kwanza ndipo afanye maamuzi, lakini pia wanaona kuwa kocha amekuwa mkali sana kwa wachezaji,”alidokeza mmoja wa viongozi wa Yanga.

Spoti Xtra ambalo linaongoza kwa mauzo kila Alhamisi na Jumapili, lilimtafuta Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Samwel Lukumay akasema; “Siku zote mwenye mamlaka ya kuteua nahodha ni kocha yeye ndiye anayejua mchezaji gani anafaa kuwa kiongozi wa wenzake.”

“Kwa hiyo tunachosubiri ni ripoti yake kuhusiana na mabadiliko hayo kwa hiyo baada yapo ndiyo tunaweza kuwa na chochote.

CHANZO: SPOTI XTRA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *