Mwanaharakati Mzalendo

WENGER AMCHANA OLE GUNNAR SOLSKJAER NA MAN UNITED BAADA YA 2-0 DHIDI YA PSG

Aliyekuwa kocha wa zamani na wa muda mrefu wa klabu ya ARSENAL ya jijini London, Bwana Arsene Wenger ameikosoa vikali timu ya Manchester United na kiwango walichokionyesha jana Jumanne usiku katika mchezo wao wa klabu bingwa Ulaya dhidi ya klabu ya PSG na kusema kuwa walipotezwa kabisa katika eneo la kiungo. 
Ole Gunnar Solskjaer jana alipata kipigo cha kwanza katika Uongozi wake katika timu hiyo toka amekabidhiwa baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo JOSE MOURINHO kuamua kuachana nayo mwishoni mwaka jana. 
Arsene Wenger anaamini mechi hiyo iliamuliwa katika eneo la katikati/kiungo huku akiongelea utofauti wa ubora uliopo katika viungo wa timu hizo mbili na kumsifu kocha wa PSG bwana Thomas Tuchel kwa kumzidi mbinu mpinzani wake. 
“Katika Ligi ya mabingwa Ulaya ni muhimu kutoruhusu kutawaliwa katika eneo la kiungo lakini Man United wairuhusu hilo litokee na wakatawaliwa katikati”, Wenger alisema hayo akiwa kituo cha televisheni cha beIN SPORTS baada ya mechi kuisha. “PSG walicheza wakiwa na viungo 5 na unaweza kuona jinsi walivyokuwa hawapotezi mipira. Man United hawakuweza kupokonya mpira kwa haraka kutoka kwa PSG na kila muda walipokuwa wanaupata walikuwa wakipoteza kwa haraka sana kwasababu PSG walikuwa wametawala eneo la kiungo”. 
 
“Pale kwenye kiungo ndipo walipopoteza mpambano ule. Unapocheza nyumbani na hauwezi kukaa na mpira muda mwingi lazima utakuwa kwenye matatizo tu na hicho ndicho kilichotokea. Man United walionekana wabovu katika kiungo ukilinganisha na uzuri wa PSG. Na pia ni kwasababu ya faida ambayo PSG walikuwa nayo ya kuchezesha viungo 5 na wachezaji wachache washambuliaji”.
Aliendelea: “Utofauti wa kimbinu, na kasi ya kuuelewa mchezo, vilikuwa vikubwa kwa timu hizi mbili kadri mchezo ulivyokuwa ukiendelea kuchezwa. Man United walikuwa wanacheza nyumbani na wamepiga shuti moja tu langoni mwa PSG kwenye mechi ya ligi ya mabingwa Ulaya, hii inakuelezea utofauti mkubwa ambao upo kati ya hizi timu 2.” 
  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *