Mwanaharakati Mzalendo

UEFA: KIPI KILICHOWAFANYA ATLETICO KUPOTEZA NA JUVENTUS KUSHINDA JANA?

Utakubaliana nami kuwa UEFA ya mwaka huu imejaa matokeo tusiyiyatarajia mengi sana. Kuanzia kwa kutolewa kwa mabingwa watetezi Real Madrid na makinda wa Ajax, kutolewa kwa Borussia Dortmund bila wao kufunga goli kwenye mechi zote 2, Kutolewa kwa PSG na Man United wakati walikuwa wakiongoza 2-0 kutoka katika mechi ya kwanza, na sasa Juventus Kupindua matokeo mbele ya Atletico Madrid. 
Wengi tuliwapa nafasi kubwa sana Atletico kwenda kulinda ushindi wao wa kwanza wa 2-0 walioupata kule Hispania na hata kupata japo goli 1 au 2 katika mechi hiyo kupitia wakali wao kama Antonio Griezmann na Alvaro Moratta. Mechi iliisha kwa matokeo ya Juventus 3-0 Atletico Madrid na kufanya Juventus wafuzu kwenda hatua ya robo fainali. 
Hebu tuangalie zipi zilikuwa sababu za Juventus kufanikiwa hapo jana na Atletico kufeli:
1. ATLETICO MADRID KUPAKI BASI:
Hii naweza kusema ndio sababu kubwa ya Atletico kupoteza mechi ya jana. Tokea dakika za mwanzo, kocha Diego simeone alikuwa akisisitiza ulinzi mkubwa kuanzia mbele hadi kwa mabeki wake. Na alifanya hivyo kwasababu alijua kuwa Juve watacheza kufa na kupona ili washinde ile mechi (watashambulia sana). Sababu nyingine iliyowafanya wacheze kwa kujilinda zaidi ni kwasababu walikuwa wana faida ya goli 2 walizozipata kule Hispania. 
Wachezaji wa Atletico Madrid wakihuzunika mara baada ya kuruhusu goli la kwanza la CR7 hapo jana.
Kukaba kwao sana kuliwafanya washindwe kufanya mashambulizi kabisa. Mpaka mapumziko walikuwa hawajapiga shuti japo moja tu langoni mwa Juventus. Sasa unashindaje mechi kwa takwimu butu kama hii? Mpaka mpira unaisha, Juve walikuwa wamepiga mashuti 16 huku 4 yakilenga goli, Lakini Atletico wamepiga mashuti 5 tu na HAKUNA LILILOLENGA GOLI. 
2. UWEZO BINAFSI WA CRISTIANO RONALDO:
Hakuna anayebisha juu ya uwezo wa Cristiano Ronaldo kuwa mmoja wa wachezaji wa ajabu kuwahi kutokea duniani bila kujali umri wake kwa sasa. Huyu jamaa ndiye aliyefunga magoli yote matatu hiyo jana na kuwatoa Atletico nje ya Champions League. Kama unadhani ilikuwa mara ya kwanza kwa Ronaldo kuwaumiza Atletico, basi ngoja nikufahamishe kuwa Atletico ni vibonde wakubwa wa CR7 tokea yupo LALIGA na mpaka sasa. 
Hebu angalia hizi takwimu hapa:
Takwimu za Cristiano Ronaldo dhidi ya Atletico Madrid
Ronaldo alicheza kama mchezaji mwenye uzoefu na michuano hiyo hapo jana na alikuwa akiwahamasisha wenzake pia kupambana mpaka wakapata matokeo. Magoli aliyoyafunga yanaonyesha jinsi gani anajua anachokifanya. Ni fundi. Anajua. Pongezi kwake. 
3. MBINU ZA MAXMILIANO ALLEGRI: 
Najua CR7 ametawala vichwa vya habari ( Anastahili ) lakini naamini kwa kiasi kikubwa sana huyu mwanaume ‘ Federico Bernardeschi ‘ alikuwa ndimu na chumvi kwa wakati huo huo kwenye ushindi wa jana na pongezi za mabadiliko ya kimbinu zimuendee kocha Maxi Allegri hasa pia kwa kuwa na uthubutu wa kumuacha nje Paulo Dybala na kuanza uwanjani na muitaliano huyo.
Dhumuni kubwa ni kutanua uwanja kuwafanya Atletico kuzuia sehemu kubwa ya uwanja , kumuwezesha Federico Bernardeschi kupiga krosi nyingi sana kutoka wingi zote mbili ili CR7 na Mandzukic wafaidike na mipira ya juu, kwa kuwa mechi ya kwanza walicheza ‘Narrow’ sana yaani CR7, Mario na Dybala wote walikuwa wanatoka katikati (Dybala akicheza nyuma yao), iliwarahisishia ukabaji Atletico. 
Kocha wa Juventus Massimiliano Allegri akimpongeza CR7 akiwa anatoka uwanjani
Lakini jana Allegri akaamua ku-take risks na kumuacha Dybala nje na kuanza na Federico Bernardeschi. Imemlipa kweli kweli. 
4. NJAA YA JUVENTUS KUCHUKUA UBINGWA WA LIGI YA MABINGWA ULAYA: 
Kama ulikuwa haujajua sababu kuu ya Cristiano Ronaldo kusajiliwa na JUVENTUS basi leo ngoja nikwambie. Ni kushinda ligi ya mabingwa Ulaya. Ronaldo anaijua hii michuano. Amechukua mara 5 akiwa na timu 2 tofauti na makocha 3 tofauti. Pia ni kama ana ‘KISMATI’ na michuano hii. Yaani anaweza asifunge kwenye ligi kuu au timu ya taifa, lakini ikija mechi ya UEFA anakuwa mnyama wa tofauti kabisa. 
Mashabiki wa Juventus wakishangilia na kuipa sapoti timu yao katika moja ya mechi zao
Juventus wanalitaka kombe hili kwa udi na uvumba. Wamechoka kuwa timu ya kuingia fainali na kutolewa mara kadhaa kwa miaka ya hivi karibuni. mwaka 2015 waliingia fainali wakakutana na Fc Barcelona wakachapwa 3-1, Barca wakabeba kombe. Mwaka 2017 waliingia fainali wakakutana na Real Madrid, wakapigwa goli 4 wakarudi Turin kulala. 
Mashabiki wa JUVENTUS wamechoka kila mwaka kuchukua makombe ya ligi na sasa wanataka UEFA Champions League. 
5. KIWANGO CHA CHINI WALICHOONYESHA WACHEZAJI WA KUTEGEMEWA WA ATLETICO MADRID:
Vyombo vya habari vingi vilivyotoa RATINGS za wachezaji waliocheza jana wanaweza wakathibitisha hii point yangu. Safu ya Ulinzi ya Atletico ilikuwa ikifanya makosa zaidi jana kuliko ile ya kule Hispania wiki 2 zilizopita.

Kule Hispania walimkaba vyema Ronaldo na hakufurukuta kabisa. Hivyo hivyo kwa Mandzukic na Dybala pamoja na viungo wote wa Juventus. Ila jana Ronaldo alikuwa Free sana, Pjanic ndio usiseme. Antonio Griezmann hakufanya la maana lolote jana, Alvaro Morata ambaye anaijua Juve kwani alishawahi kuwa mchezaji wao, pia hakufanya la maana, beki Juafran hakufanya la maana, Diego Godin makali yake jana hayakuonekana.

Antonio Griezmann akionyesha kutofurahishwa na yaliyokuwa yakitokea mchezoni hapo jana

Hizi ni baadhi ya Ratings walizopewa wachezaji wa Atletico:
Oblak (7/10*); Arias (5/10), Godin (6/10), Gimenez (6/10), Juanfran (5/10); Saul (6/10), Rodri (6/10), Koke (6/10), Lemar (6/10); Griezmann (6/10), Morata (6/10). 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *