Mwanaharakati Mzalendo

Dkt. John Pallangyo ashinda kura za maoni CCM kurithi kiti cha Nassari


Pallangyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi(CCM) mkoani Arusha, ameshinda kwa kishindo kinyang’anyiro cha kura za maoni ndani ya chama hicho kwa ajili ya kupata mkombea Ubunge katika jimbo la Arumeru.

Uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo lililokuwa likishikiliwa na Joshua Nassari wa Chadema, umepangwa kufanyika Mei 19 mwaka huu, baada ya Mahakama ya Kuu Kanda ya Dodoma kutupilia mbali kesi iliyofunguliwa na Nassari la kupinga kung’olewa kwenye nafasi hiyo.

Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza jimbo hilo kuwa wazi baada ya Nassari kushindwa kuhudhuria vikao vitatu vya Bunge mfululizo bila kutoa taarifa kinyume cha kanuni.
Katika uchaguzi huo uliofanyika jana katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, wagombea 33 wakiwamo wanawake watatu, walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania kuteuliwa na chama hicho.

Akitangaza matokea hayo, msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, ambaye pia ni mlezi wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Humphrey Polepole,
alisema kati ya kura 690 zilizopigwa, Dk. Pallangyo aliibuka mshindi kwa kupata kura 470.
Polepole alisema mshindi wa pili ni Wakili Dk. Daniel Pallangyo, aliyepata kura 50 huku William Sarakikya akishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 36.

Alisema wagombea wengine walipata kura kuanzia 26 hadi sifuri si kwamba hawana sifa za kuwa wagombea ubunge na kwamba kura alizopata mshindi wa kwanza si kigezo cha kumfanya awe mgombea
wa CCM kwa sababu bado kuna vikao vya kujadili wagombea hao na majina yote yatajadiliwa.


”Wagombea wote bado mna sifa za kuwa wagombea ubunge kwa sababu vikao bado vipo vingi vya kujadili majina haya kwa kina ikiwa ni pamoja na kuchunguza kama mgombea aliyepata kura nyingi amezipata kwa njia halali,” alisema.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Arumeru, Shaaban Mdoe, alisema wagombea wote walikubaliana na matokeo hayo ambapo kila mmoja alisaini na kuridhika kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.

Aidha, aliwataka wagombea hao wakati wakiendelea kusubiri vikao vya maamuzi kutofanya kampeni za aina yeyote ile wala kuchafuana kwa njia yeyote kwa sababu bado mchakato ni mrefu wa kuwajadili kwenye vikao ndani ya CCM.

Mdoe alitoa rai kwa wana CCM wilayani humo kukubaliana na mgombea atakayeletwa kupeperusha bendera ya CCM baada ya vikao vya uteuzi kumaliza kazi yake.

”CCM haina mtoto wa mgongoni wala wa tumboni wagombea wote ni sawa hivyo niwaombe wana CCM wenzangu kuepuka kuwa na makundi wakati wa
kampeni na badala yake washirikiane na uongozi kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo,” alisema.
Akizungumza baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi huo, Dk. Pallangyo aliwashukuru wana CCM wote waliomwamini na kumpa kura nyingi zilizompa ushindi wa kishindo na kwamba uchaguzi huo ulikuwa wa huru na haki.
”Nawashukuru wana CCM wenzangu kwa kuniamini na kunipa ushindi wa kishindo uchaguzi ulikuwa wa haki kura zimehesabiwa bila changamoto
yeyote na wagombea wezangu wameridhika na kukubali kusaini matokeo ya uchaguzi huu,” alisema.
Katika uchaguzi huo, ulinzi uliimarishwa nje na ndani ya ukumbi lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna makada wanaoingia kwenye eneo hilo ambao walikuwa siyo wajumbe wa mkutano huo mkuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *