Mwanaharakati Mzalendo

WEZI WAIBA VITO VYA DHAHABU KATIKA JUMBA LA MENGI

Siku tatu baada ya mfanyabiashara tajiri wa Tanzania marehemu Reginald Abraham Mengi kuzikwa, wezi wameibia familia yake ambayo bado inaomboleza vifaa vya thamani na fedha taslimu mjini Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi vitu vinavyodaiwa kuibiwa ni pamoja na mikufu ya dhahabu, kompyuta pamoja na fedha taslimu ambazo kiwango chake hakijaelezwa.

Vitu hivyo vinasemekana kuwa ni mali ya familia na waombolezaji na zilikuwa katika jumba la kifahari la mjane wake, Jacqueline Mengi ambako mwenyekiti huyo wa kampuni za IPP alizikwa Alhamisi iliyopita.

“Ni kweli nyumbani kwa Mengi kumeibiwa,” alisema Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah na kuthibitisha kuwa wanawashikilia watu wawili wanaoshukiwa kuhusika na wizi huo.

Kamanda Issah pia ameongeza kuwa tukio hilo huenda limefanywa na watu wanaodaiwa kuwa wa ndani na familia hiyo na kwamba taarifa zaa awali za uchunguzi zinaonyesha walitokea jijini Dar es Salaam.

“Suala hilo ni la ndani na tukianza kulishughulikia kikamilifu litahusisha watu ambao ni wa ndani. Sasa sijui tutakuwa kwenye msiba au tutakuwa tunakamatana, maana tumeongeza huzuni juu ya huzuni”.

Akizungumza na Gazeti la Mwananchi Kamanda Issah alisema kuwa kulitokea watu mchanganyiko wakati wa mazishi ya Bw. Mengi na kila mtu alisema yeye ni mwanafamilia na ”kila mtu anaingia mahali ambako hahusiki na matokeo yake ni wizi.”

Alisema baadhi ya watu ambao hawakutaka majina yao yatajwe, walidai baadhi ya waliohusika walikuwa wamevalia vitambulisho vilivyoandikwa IPP.

Msemaji wa familia hiyo, Benson Mengi alisema kwa sasa hawawezi kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa bado uchunguzi unaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *