Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekanusha taarifa za upotoshaji zilizochapishwa katika magazeti mawili ya jana Juni 17, 2019.
Taarifa hizo zilizochapwa katika gazeti la FAHARI YETU toleo Na 163 la Jumatatu Juni 17, 2019 ukurasa wa kwanza ikiwa na kichwa cha habari VIRUSI WA RUSHWA NDANI YA TAKUKURU HAWA HAPA’ pamoja na Gazeti la TANZANITE Toleo Naa 478 la Jumatatu Juni 17, 2019 ukurasa wa kwanza ikiwa na kichwa cha habari MTANDAO HATARI WA RUSHWA NDANI YA TAKUKURU WABAINIKA’.
TAKUKURU wameufahamisha umma kwamba taarifa hizo ambazo zimeandikwa kwa kufanana katika magazeti yote mawili ni za upotoshaji wenye lengo la kudhoofisha utendaji kazi wa TAKUKURU hasa katika kipindi hiki cha mapambano na wakwepa kodi, wabadhirifu wa mali za umma pamoja na wahujumu wa uchumi.
Katika taarifa yao kwa umma TAKUKURU wamesema kuwa wanafahamu fika kwamba wapo vitani na kwamba kadri wanavyoongeza kasi ya mapambano ndivyo vivo hivyo ambavyo wala rushwa pamoja na wanaonufaika na vitendo vya rushwa wanaendelea kutafuta mbinu za kudhoofisha mapambano dhidi ya rushwa na kuwakatisha tamaa watumishi wao.
Walimalizia kwa kusema kuwa wanapenda kuuhakikishia umma kwamba TAKUKURU ipo imara na itaendelea kuwafichua na kuwashughulikia kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nan 11 ya Mwaka 2007, wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa bila ya kujali cheo, wadhifa, jinsia wala itikadi.