DKT. BASHIRU: JIMBO LA HAI SI NGOME YA CHADEMA

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ametaja sababu ya ziara yake mkoani Kilimanjaro kuanzia Wilaya ya Hai lilipo jimbo la Hai ambalo mbunge wake ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Amesema ameanzia Hai kimkakati kwa maelezo kuwa jimbo hilo si ngome ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.
Ametoa kauli hiyo jana Jumapili Julai 7, 2019 katika kikao cha ndani kilichofanyika katika uwanja
wa Sabasaba.
“Katika Mkoa wa kilimanjaro nimepanga kupita wilaya kwa wilaya kwa sababu ya uzito na umuhimu. Nimeanzia Hai kimkakati na mahesabu yametumika kuamua kuanzia Hai katika ziara yangu,” amesema Dk Bashiru.
Katibu mkuu huyo ametoa maelekezo kwa mabalozi kupewa nafasi katika mikutano pindi wanapofika viongozi wa kitaifa mikoani.
Naye katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya, amesema mwaka 2015 chama hicho kilipoteza majimbo kadhaa mkoani Kilimanjaro kutokana na makundi baada ya kumalizika kwa kura za maoni.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM iliibuka na ushindi katika majimbo mawili kati ya tisa mkoani humo na madiwani 52 kati ya 169.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *