Mwanaharakati Mzalendo

MAHAKAMA KUU ZANZIBAR KUFUTA KESI ZISIZOKAMILIKA USHAHIDI

Mahakama Kuu ya Zanzibar imesema itazifuta kesi ambazo upelelezi wake umechukua muda mrefu bila ya kukamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar, Mrajis wa Mahkama kuu Zanzibar Mohamed Ali Mohamed alisema zipo kesi kila zinapoitishwa mahakamani huelezwa upelelezi haujakaamilika.
Alibainisha kuwa ziara iliyofanywa hivi karibuni na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, katika Vyuo vya Mafunzo amebaini mrundikano wa mahabusu unatokana na kusita kuendelea kwa kesi zao mahakamani kwa kile kinachoelezwa kuwa ushahidi haujakamilika.
Alisema kurundika kwa mahabusu hasa Chuo cha Mafunzo cha Wete na Kilimani mjini Unguja kumetokana na kutoendelea kwa kesi zao zinazosubiri kwa kukamilika kwa ushahidi.
“Kesi ambazo upelelezi wake umechukua muda mrefu na usiokamilika, tutazifuta”, alisema Mrajis huyo.
Aidha Mrajis huyo alisema sababu nyengine ya uwepo wa mrundikano wa mahabusu katika Vyuo vya Mafunzo hapa Zanzibar, pia unatokana kuwekwa kwa masharti magumu ya dhamana.
Alisema atahakikisha makosa mdogo madogo na makubwa yanapatiwa dhamana isipokuwa yale makossa ambayo yamezuiwa kwa mujibu wa sheria.
Alisema hatua hiyo itapelekea kusaidia kuondoa mrundikano wa mahabusu katika Vyuo vya Mafunzo, kama ilivyobainika kwenye ziara hiyo ya Jaji Mkuu hali ambayo inawafanya kukosa haki zao za msingi.
Mohamed aliwashauri viongozi kuangalia namna ya kupitisha vifungu vya adhabu wakati wanapopitisha sheria katika mabaraza ili kuondoa athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo kupunguza masharti magumu ambayo wengine wanashindwa kutimiza masharti hayo.
Aidha alisema kutokana na ziara hiyo ya Jaji Mkuu alitoa maelekezo kwa mahakimu kuhakikisha kuwa suala la dhamana linapatiwa ufumbuzi kwa makosa madogo kwa mujibu wa sheria ili kuondosha usumbufu unaojitokeza.
Hata hivyo, alisema hali halisi ya magereza kwa Zanzibar ni nzuri kutokana na serikali kuboresha huduma pamoja na kuwajengea watoto magereza yao ili kuepuka kuchanganyika na watu wazima.
Hivyo alisema jumla ya mahabusu 262 wapo katika Vyuo vya Mafunzo ambapo wengi wapo kwa muda mrefu, sambamba na kuwataka mahakimu kurekebisha mienendo ya kesi ili kuona zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *