Mwanaharakati Mzalendo

KESI YA KUPINGA TUNDU LISSU KUVULIWA UBUNGE WA SINGIDA MASHARIKI KUAMULIWA AGOSTI 23, 2019

Maombi namba 18/2019 yanayohusu shauri la kupinga kuvuliwa Ubunge Mbunge wa Singida Mashariki, Mhe. Tundu Lissu, ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, yameanza kusikilizwa jana Alhamisi, Agosti 15, 2019 mbele ya Jaji Matupa, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam na kesi imeahirishwa hadi Agosti 23 mwaka huu.
Kupitia mawakili wanaomtetea Mhe. Lissu, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala akiwa na mawakili wenzake, Freddy Kalonga, Jeremiah Mtobesya na Omary Msemo, upande huo umeiomba Mahakama Kuu 
1. Kusimamisha uapishwaji wa mbunge mteule wa jimbo hilo, hadi shauri maombi hayo yatakaposikilizwa na kuamriwa.
2. Wameiomba Mahakama Kuu kulitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha barua rasmi yenye uamuzi wa Spika wa Bunge kufuta ubunge wa Mhe. Tundu Lissu.
3. Wameiomba Mahakama Kuu kutoa uamuzi haraka kabla mbunge huyo mteule hajaapishwa.
Aisha, upande wa mawakili wa mpeleka maombi, Tundu Lissu ambaye anawakilishwa na Ndugu Allute Mughwai, waliomba ombi la kuhusu kumtaka Spika wa Bunge asimwapishe mbunge mteule wa Jimbo la Singida Mashariki lisikilizwe leo hii. 
Upande wa Jamhuri walitaka ombi hilo lisikilizwe wakati wao wakiwa wameshawasilisha majibu yao. 
Katika ubishani huo wa kisheria, Jaji Matupa ameamuru yafuatayo:-
a) Maombi yote yatasikilizwa Agosti 23, mwaka huu. 
b) Upande wa Jamhuri (wajibu maombi) walete majibu yao Agosti 21, 2019.
c) Upande wa wapeleka maombi walete majibu yao ya nyongeza Agosti 22, 2019.
d) Baada ya usikilizwaji wa Agosti 23, mwaka huu, ndipo uamuzi wa hoja/maombi yote ya wapeleka maombi utakapotolewa.
Jaji Matupa amesema amefanya “consultations” kwamba kabla ya Agosti 23, mwaka huu hakuna kikao cha Bunge na kwamba mbunge huyo mteule hatakuwa ameapishwa katika kipindi hiki.
Upande wa wajibu maombi (Jamhuri) waliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Vincent Tangoh na mawakili wenzake, Lucas Malunde na Mark Mulwando.
Hivyo Jaji wa Mahakama Kuu Sirilius Matupa ameaihirisha kesi hiyo hadi Agosti 23 mwaka huu.
Wakati huo huo, kesi namba 112/2018 inayowakabili baadhi ya Viongozi Wakuu wa Chama na Wabunge 7 wa Chadema katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyokuwa iendelee leo, imeahirishwa hadi Jumatatu Agosti 19, mwaka huu. Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya Wakili Gaston Garubindi, kutoa taarifa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Simba, kwa niaba ya mawakili wanaowatetea washtakiwa katika shauri hilo kuwa, mawakili hao wako kwenye kesi nyingine mahakama ya juu, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuwakilisha upande wa wapeleka maombi (utetezi) katika maombi namba 18/2019 yanayohusu shauri lililofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Chama, Mhe. Tundu Lissu dhidi ya Spika wa Bunge, kupinga kuvuliwa Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *