Mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari ya Arusha Meru mwenye Asili ya Kiasia Faisal Ibrahim 19 mkazi wa kata ya kati jijini Arusha amejipiga risasi kichwani kwenye paji la uso akiwa chumbani kwake.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoani hapa Jonathan Shana alisema kuwa mwanafunzi huyo alijipiga risasi kwa kutumia bunduki aina ya Rifle Winchester inayomilikiwa na mzazi wake aitwaye Sallim Ibrahim miaka 56.
Alisema kuwa marehemu ambaye huishi na wazazi wake kwenye nyumba za shirika la nyumba la taifa NHC iliyopo plot namba 3 na nne eneo la soko kuu jijini Arusha alfajiri saa kumi na moja alijipiga risasi kwenye paji la uso na kusababisha kifo chake.
Ameeleza kuwa taarifa za awali zinaeleza kuwa chanzo cha kifo hicho kinatokana na msongo wa mawazo uliotokana na matumizi ya dawa za kulevya yaliopelekea kuchukuwa maamuzi hayo ya kujiuwa.
Akatoa wito kwa kwa wamiliki wa silaha mkoani hapa kuzitumia kwa umakini mkubwa na pia kuzitunza mahala salama ili kuepusha madhara ambapo sio rahisi kwa mtu au mtoto yeyote kuzifikia na mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye Hospital ya mkoa ya Mount meru ukisubiri hatua za uchunguzi.
Kamanda Shana alisema kuwa katika tukio hilo hakuna mtu yoyote anayeshikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo .