Mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya Msingi Osunyai, Elibariki Lekine (12) mkazi wa Muriet jijini Arusha amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya katani.
Tukio hilo limethibitishwa na kamanda wa polisi Mkoani humo, Jonathan Shana ambapo alidai kuwa limetokea Jana majira ya SAA 11:28 jioni katika mtaa wa FFU kata ya Muriet jijini Arusha.
Kamanda shana alisema mwili huo ulikutwa kwenye nyumba ambayo ujenzi wake unaendelea inayomilikiwa na Emmanuel Thomas mkazi wa eneo hilo.
Aidha alisema mwili huo ulikutwa unaning’inia juu huku kamba iliyotumika ilikuwa imefungwa kwenye mbao ya jukwaa linalotumiwa na mafundi ujenzi.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya upelelezi juu ya tukio hilo ili kuweza kujua chanzo halisi cha tukio hilo na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru kwa uchunguzi zaidi.