Rais wa Italia Sergio Mattarella amempa Waziri Mkuu Giuseppe Conte agizo la kuunda serikali mpya Alhamisi, kufuatia mpango wa kuepusha uchaguzi wa mapema.
Uamuzi huo umetolewa na Mattarella baada ya vyama viwili vya kisiasa nchini Italia, kile Nyota Tano na cha Democratic, kukubaliana kuunda serikali mpya ya mseto. Vyama hivyo vimeamua kuweka kando tofauti zao kuepusha uchaguzi ambao unaweza kumpa ushindi waziri wa mambo ya ndani wa siasa kali za mrengo wa kulia Matteo Salvini kama Waziri Mkuu.
Muungano huo utaongozwa na waziri mkuu anayemaliza muda wake Giuseppe Conte, ambaye alijiuzulu wiki iliyopita kufuatia kuanguka kwa serikali yake mapema mwezi huu baada ya kukosa uungwaji mkono wa chama cha Salvini cha League.
Conte amelikubali agizo hilo na anatapewa siku chache za kufanya mashauri ya kisiasa kuhakikisha wingi kuhakikisha kwamba anapata wingi wa viti bungeni. Conte atahitaji kushinda kura ya imani kurudi tena madarakani kama Waziri Mkuu. Akipokea agizo hilo Conte lisema yafuatayo:
“Mimi ni profesa na wakili. Katika maisha yangu nimetetea watu wengi, sasa najitolea kutetea masilahi ya Waitaliano wote katika maeneo yote,” amesema Conte.
Kiongozi wa Chama cha Nyota Tano Luigi Di Maio amesema mpango huo na chama cha Democratic utalazimika kupitishwa na wanachama wa chama chake kwa kura ya mtandaoni, ambayo inaweza kufanywa wikendi hii.