Diamond, Harmonize kukutana Dubai?


Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku mbili kufanyika kwa tamasha la muziki Dubai kwa kuwakutanisha wasanii nyota mbalimbali wa Afrika, maswali ni je wasanii wa Tanzania Diamond platnumz na Harmonize wataweza kukutana huko.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Ijumaa Novemba 15, 2019 katika ukumbi wa matamasha wa ‘Festival Arena’ ambapo wasanii zaidi ya 18 watalishambulia jukwaa.
Wasanii wanaotarajiwa kupanda jukwaani siku hiyo ni pamoja na Wizkid, Burna Boy, Teni, Tekno, Tiwa Savage, 2 Face, Jah Prayzah, Akothee, na Betty G.
Wengine ni  Lij Michael, Khatty Man, Nandy Diamond Platinumz, Harmonize, Eddy Kenzo, Souhila na The Ben.
Hata hivyo, wasiwasi upo kama wasanii hao wa Tanzania Diamond Platnumz na Harmonize kama watakutana ukizingatia ni wiki mbili zimepita tangu walipotarajiwa kuwepo kwenye utoaji tuzo za African Muzik Magazine Award (AFRIMMA) zilizotolewa mji wa Dallas Jimbo la Texas nchini Marekani lakini hawakutokea.
Katika tuzo hizo mbali ya Diamond kuwa mteule katika tuzo hizo kupitia kipengele cha msanii bora wa kiume Afrika Mashariki ambapo Omy Dimpozi alishinda, pia alikuwa mmoja wa wasanii ambao wangetakiwa kutumbuiza siku hiyo.
Hata hivyo sio Diamond wala Harmonize waliotokea katika usiku wa tuzo hizo.
Hivyo kufanyika kwa tamasha hili la Dubai nalo linaleta maswali kama wawili hao watakutana au la, ukizingatia hawajawahi kuonekana wakiwa pamoja tangu pale uongozi wa Wasafi ulipoeleza Harmonize kutaka kuvunja mkataba wa kuwa chini ya lebo yao ambapo mwenyewe alisema anatakiwa kuwalipa Sh500 milioni ili kuachana nao.
Tayari Diamond kupitia akaunti yake ya Instagram amekwisha kudhibitisha kwamba atahudhuria tamasha hilo huko Harmonize akiwa amealikwa lakini bado hajathibitisha kama atakuwapo au la.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *