Mwanaharakati Mzalendo

KUPOTEZA KWA WAWAKILISHI WETU KIMATAIFA IWE SOMO KWA WAKATI UJAO, KAZI SASA NDANI YA LIGI


TAYARI kwa wawakilishi wetu wa kimataifa Yanga kwenye Kombe la Shirikisho wamefungashiwa virago jumla nao watabaki kuwa watazamaji kama ilivyo kwa wawakilishi wetu waliopita.

Mchezo wao wa mwisho ambao ulikuwa umeshikilia tiketi yao ya kutinga hatua ya makundi ulikamilika kwa kupoteza kwa kufungwa mabao 3-0 jambo ambalo limezima ndoto zao kimataifa.

Kwa maana hiyo Yanga imetolewa hatua ya mtoano kwa jumla ya mabao 5-1 kwa kuwa mchezo wa kwanza uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba ilikubali kupoteza kwa kufungwa mabao 2-1.

Hatua ambayo wamefikia kwa msimu huu sio mbaya na sio nzuri kwa kuwa hawajatimiza malengo waliyojiwekea kuweza kufuzu hatua ya makundi.

Kutolewa kwao kwenye hatua hii ugenini inatakiwa iwe somo kwa wakati mwingine kujiandaa na kutumia vema mechi za mwanzo hasa zile zinazochezwa nyumbani.

Kupoteza haina maana kwamba hamjaonyesha ushindani hapana nimeona namna ambavyo Yanga ilicheza mchezo wa marudio haijafanya vibaya ilipambana.

Makosa yapo kwenye mpira na kupoteza ni sehemu ya matokeo ambayo yanapaswa yapokelewa na mashabiki pamoja na Taifa ingawa ni maumivu makubwa.

Wawakilishi wetu mmepambana hilo lipo wazi kwani kufungwa mabao 3-0 ugenini hiyo ni dalili kwamba mmeanza kutengeneza muunganiko mzuri wa kikosi.

Tumeona namna Yanga ilivyocheza bila ya uwepo wa beki mkongwe Kelvin Yondani ambaye alikuwa na kadi nyekundu.

Muunganiko umeanza kuonekana ingawa kikosi hakijashinda ni sehemu ya kuanza kushikilia hapo na kufanya mabadiliko makubwa kwenye usimamiaji wa kikosi.

Mchezo wa kwanza uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba Yanga inaonekana haikuwa tayari kushinda bali ilikuwa inajilinda ndio maana mfumo mkubwa uliotumika ulikua ni kujilinda.

Mtindo wa kujilinda ukiwa nyumbani ni mzuri ikiwa inatokea tayari timu imeshinda zaidi ya mabao 3 hapo ndipo inapokuwa sawa kwa wachezaji kubadili mbinu na kuanza kujilinda.

Kukosea kulianza nyumbani ndio maana mchezo wa pili kulikuwa na utofauti kidogo uliofanya timu ikachangamka licha ya kupoteza kwa kufungwa mabao 3-0.

Mchezo wa pili Yanga ilifunguka mwanzo mwisho na ilionesha nia ya kutafuta matokeo jambo lililoleta upinzani kwa wapinzani wao Pyramids FC.

Mmezidiwa kwa makosa mnapaswa msijilaumu sana matokeo ya mpira wakati mwingine huwa ya kuumiza ni lazima kuyakubali na kuendelea kujipanga upya.

Mfumo wa Yanga ambao umekuwa ukitumika ndio chanzo cha timu kushindwa kushinda endapo mabadiliko yatafanyika kwenye mfumo basi wakati ujao Yanga itafanya vizuri kimataifa.

Jambo lingine ambalo limekuwa ni mwiba kwa Yanga kwenye mechi za nyumbani ni ile hali ya kucheza kwa kupania wakiwa nyumbani.

Kucheza kwa presha kubwa ya mashabiki kumekuwa kukiwapotezea umakini katika hili wanatakiwa wajiandae kisaikolojia kwani wakiruhusu hali hii iendelee itawamaliza na kwenye ligi pia.

Presha ya mashabiki ni nzuri pale inapotafsiriwa kwa matokeo chanya na wachezaji wenyewe pamoja na benchi la ufundi ila pale ambapo wanashindwa kujizuia ni mbaya.

Wachezaji wakiruhusu kucheza kwa kuwafuata mashabiki wa kwenye jukwaa inawamaliza na kuwafanya washindwe kupata matokeo.

Hakuna namna  yaliyotokea Misri yamepita na lazima kila mmoja akubali hali halisi ili kuendeleza maisha ya harakati kutafuta mafanikio.

Wale ambao bado wana maumivu kutokana na kupoteza wanapaswa wajifunze kwamba mpira hautabiriki na hakuna ambaye atadumu akiwa mchezaji maisha yake yote.

Kama ilivyokuwa awali kila mmoja alikuwa na morali ya kufanya kazi lakini mwisho wa siku wengi wamepoteza dira ambayo walijiwekea.

Kwa sasa ni wakati wa kutazama maisha mengine kwenye Ligi Kuu Bara ambayo moto wake unazidi kushika kasi.

Kila timu imejipanga kufanya vema jambo hilo na liwe hivyo kwa timu zote kuleta ushindani bila kujali inacheza na timu gani.

Wakati mwingine timu zetu zikipata nafasi kushiriki michuano ya kimataifa ni lazima zijipange sawa kuleta ushindani wa kweli na kufika hatua ya mbali.

Yote yanawezekana iwapo timu zitaanza mipango yao kwa wakati ili kupunguza stress za maisha na soka.

Tumeambulia patupu kwenye michuano ya kimataifa licha ya kuwa na timu nne ambazo zilikuwa zinawakilisha nchi yetu kimataifa. 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *