Mwanaharakati Mzalendo

MDEE NA WENZAKE WATOA SABABU ZA KUTOKUFIKA MAHAKAMANI.

Wabunge wanne wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi, John Heche, Mchungaji Peter Msigwa, Halima Mdee na Ester Bulaya leo wameiomba mahakama isiwafutie dhamana baada ya washtakiwa hao
kujieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba wakifikishwa Mahakamani hapo kutokea Kituo cha Polisi Osterbay.

Wabunge wameiomba mahakama isiwafutie  dhamana kwa kutoa sababu mbalimbali akianza Msigwa aliomba radhi kwamba haikuwa nia yake kuidharau mahakama, tangu kesi ianze hajawahi kuchelewa, hajawahi kukaidi amri ya mahakama na kwamba anaheshimu kiti cha hakimu.

Amedai alitokea Dodoma alidhani kesi ni saa nne na nusu kama kawaida akiwa na Heche lakini walipofika walikuta kesi imeisha na jitihada za kumuona hakimu kumaliza tatizo hilo zilishindikana.

Kwa upande wake Mdee pia ameomba radhi, ameonyesha jinsi anavyoiheshimu mahakama na kwamba alichelewa kwa kuwa alipitia kupima presha zahanati na alipofika kesi ikawa imeisha na amri imeshatolewa na wadhamini wake waliwahi lakini hawakufanikiwa kumaliza tatizo hilo Novemba 15 kwa kuwa waliambiwa amri ilishatolewa.

Heche amedai aliomba asifutiwe dhamana, anadai anaheshimu mahakama, hajawahi kuidharau, siku ya kesi ilikuwa Dar es Salaam lakini alijua kama kawaida kesi yao inasikilizwa saa nne na nusu hivyo alipofika alikuta imeahirishwa.

Kwa upande wa Ester Bulaya amedai Novemba 14 alienda msibani Singida kumzika mama yake mdogo lakini aliwapa taarifa wadhamini wake ambao siku ya kesi walikuwepo katika eneo la mahakama.

Baada ya washtakiwa hao kujieleza bado mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja kisha mahakama itoe uamuzi wa kuwafutia dhamana ama la.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *