Mwanaharakati Mzalendo

SBL yahimiza usalama barabarani kueleke msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka

Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa kampuni ya Bia ya Serengeti, John Wanyancha( kushoto) akizungumza na waendesha boda boda mjini Moshi leo, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Usinywe na Kuendesha’ inayolenga kupambana na ajali za barabarani. Wengine ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani  mkoa wa Kilimanjaro, Zauda Mohamed (mbele kulia) na Mratibu wa Mafunzo Ofisi ya  Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa huo, Insp. Hamadi Hoza.

Mwenyekiti wa Bodaboda Manispaa ya Moshi,Hamad Bendera akizungumza na waendesha boda boda mjini Moshi leo, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Usinywe na Kuendesha’ inayolenga kupambana na ajali za barabarani. Wengine wanaosikiliza ni Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa kampuni ya Bia ya Serengeti, John Wanyancha (kushoto),  Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani  mkoa wa Kilimanjaro,Zauda Mohamed (mbele kulia) na Mratibu wa Mafunzo Ofisi ya  Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa huo, Insp. Hamadi Hoza.


Moshi, Novemba 14, 2019: Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) leo imetoa vifaa mbali mbali vya usalama barabarani pamoja na elimu kwa madereva wa mabasi na waendesha boda boda mjini Moshi, ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika kupambana na ajali za barabarani 


Hatua hiyo ni muendelezo wa kampeni ya nchi nzima ya kampuni ya SBL kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara na hususani madereva inayojulikana kama ‘Usitumie Kilevi na Kuendesha Chombo cha Moto’ inayohamasisha madereva kuepuka kuendesha vyombo vya moto wanapokuwa wametumia kilevi.
Utoaji huo wa vifaa ulifanywa na Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa kampuni hiyo, John Wanyancha na kushuhudiwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani  mkoa wa Kilimanjaro, Zauda Mohamed. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na makoti ya usalama barabarani, stika, vipeperushi vyenye ujumbe juu ya usalama barabarani pamoja na programu za elimu zilizotolewa kupitia redio na kwenye vyuo vya elimu ya juu vilivyopo mjini Moshi.


“Tunapoelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, kampuni ya SBL inapenda kuwakumbusha wateja wake na umma kwa ujumla kusherehekea sikukuu zinazokuja kistarabu kwa kuhakikisha hawaendeshi vyombo vya moto baada ya kutumia kilevi,” alisema Wanyancha


Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kilimanjaro aliishukuru kampuni ya SBL kwa kuandaa kampeni hiyo na kuongeza kuwa kwa kulishirikisha jeshi la Polisi kampuni hiyo inaiunga mkono Serikali katika kutoa elimu ya usalama barabarani na pia kupambana na ajali zinazosababishwa na unywaji usio wa kistarabu.


Kamanda Zauda aliwaonya madereva na watumiaji wengine wa barabara wanaotumia kilevi na kuendesha vyombo vya moto  bila kufikiria athari za kufanya hivyo na kusisitiza kuwa jeshi la Polisi halitawavumilia watu wa aina hiyo haswa katika kipindi hiki tunapoelekea msimu wa sikukuu.

 “Tunapenda kuona barabara zetu zinaendelea kubaki salama kwa kipindi chote cha msimu wa sikukuu. Hatupendi kuona uharibifu wa mali, majeruhi au mtu kupoteza maisha kwa sababu ya ajali zinazosababishwa na utumiaji pombe usio wa kistarabu na sababu nyinginezo,” alisema Zauda.


MWISHO……


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *