Nteghenjwa Hosseah, Karatu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Mb) ameagiza shilingi Milioni 70 zilizopelekwa Halmashauri ya Karatu Januari kutoka katika Mradi wa Lipa kutokana na Matokeo “EP4R” 2019 zikajenge Bweni katika shule ya Sekondari ya Wavulana ya Karatu.
Jafo ametoa kauli hiyo mapema leo alipokua ziarani Wilayani Karatu na kukagua miundombinu ya shule ya wavulana Karatu na kubaini uchakavu wa miundombinu pamoja na msongamano wa wanafunzi katika mabweni.
“Kuna Fedha zililetwa hapa Karatu tangu Januari mwaka Jana kwa ajili ya ujenzi wa vyumba za madarasa katika moja ya shule za hapa lakini hazijatumika mpaka leo sasa naelekeza fedha hizo ziletwe hapa Karatu Sekondari na ujenzi wa bweni uanze Jumatano ya wiki ijayo” amesema.
Aliongeza kuwa mara ujenzi huo utakapoanza anataka atumiwe picha zinazoonyesha shughuli za ujenzi wa bweni hilo ukiwa unaendelea.
“Shule hii ni chakavu sana na wanafunzi bado wanajitajidi kwa kufanya vizuri sasa matatizo haya yamefika mwisho ziletwe izo mil 70 kwa kuanzia huku tukiendelea kuangalia namna ya kupata fedha zaidi kwa ajili ya ukarabati mkubwa” alisema Jafo.
Akizungumza na wanafunzi shuleni hapo Waziri Jafo aliwataka wanafunzi kuongeza jitihada katika masomo na kuhakikisha wanaingia katika shule 50 bora katika mtihani wa kidato cha sita wa mwaka huu na kuwaahidi kuwa mgeni rasmi katika mahafali yao.