Taifa la Ivory Coast limeingia kwenye majonzi mazito baada ya kumpoteza waziri mkuu wa serikali hiyo, hayati Amadou Gon Colibaly aliyefariki mnamo jana jumatano kwa maradhi ya moyo.
Hayati Colibaly ambaye amehudumu kwa nafasi ya waziri mkuu tangu mwaka 2017 chini ya Rais Alassane Outarra amefariki mapema jana muda mfupi baada ya kutoka kwenye kikao cha baraza la mawaziri. Kabla ya kuwa waziri mkuu, hayati Colibaly amewahi pia kuhudumu kwa nafasi ya katibu mkuu kiongozi na pia waziri wa kilimo katika serikali ya Ivory Coast.
Kifo cha Colibaly kimeleta sintofahamu kubwa hasa kwa kuwa tayari alikuwa ameteuliwa na chama tawala cha nchi hiyo kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mnamo mwezi oktoba mwaka huu baada ya Rais aliyopo madarakani, Alessane Ouattara kusema kuwa hatowania muhula wa tatu.