Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt. Suleiman Serera ametoa wito kwa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR) kufanya utafiti wa kina kwenye Dawa zao wanazozizalisha ili kubaini kama zimeleta tija husika ya kutatua maradhi yanayowakabili Binadamu.
Ameyasema hayo katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo nchini alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge yaliyofanyika jana tarehe 27 Novemba kwenye eneo maarufu la Nyerere Square, jijini Dodoma ambapo amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kujua namna dawa wanazozizalisha zimeleta tija.
Dkt. Serera alieleza katika maadhimisho hayo kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inalenga zaidi katika kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma za afya ya Binadamu kwa lengo la kuwezesha kila Mtanzania awe na afya bora hivyo kuwasisitiza NIMR kujikita zaidi na tafiti zinazohusu magonjwa yanayowakabili Watanzania ili wawaelimishe kujikinga kuyaepuka kuliko kusubiri tiba na hatimaye kutekeleza malengo ya Serikali ipasavyo.
Katika maadhimisho hayo Wananchi wa Jiji la Dodoma walijitokeza kwa wingi katika zoezi la kuchangia damu na kupata huduma za uchunguzi wa afya zao bure uliofanywa na Taasisi ya NIMR.