Mashindano maarufu ya mbio za mitumbwi (Tanzania Boat Race) yanayoandaliwa na kampuni ya The Scope yatafanyika Desemba 13 mwaka huu, mkoani Mwanza na yanatarajiwa kujumuisha zaidi ya timu 40 za wavuvi mkoani hapa na kutoka Wilaya za Ilemela, Nyamagana, Ukerewe, Buchosa, Sengerema na visiwa vilivyopo kwenye Ziwa Victoria jirani na mkoa wa Mwanza.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mashindano haya msimu wa mwaka 2020, Meneja wa The Scope, Herbert Rweikiza, alisema Mashindano haya yataweza kufanyika kutokana na jitihada za wadau mbalimbali ambao ni Chama Cha Wapiga Makasia (Mwanza), Ofisi ya Afisa Utamaduni (Jiji la Mwanza), Umoja wa Wafanyabiashara wa Soko la Mwaloni na kampuni ya TBL kupitia kinywaji cha Balimi Extra Lager.
“Mashindano haya adimu yatakuwa endelevu na kufanyika kila mwaka, mwaka huu yatafanyika mkoani Mwanza na mwakani yatajumuisha mikoa yote ya kanda ya ziwa ambayo ni Mwanza, Mara, Simiyu, Geita, Kagera na Kigoma kwa upande wa ziwa Tanganyika na tunatarajia kuyaboresha zaidi mwaka hadi mwaka ili yawe na mvuto zaidi na kushirikisha washindani wengi na wadau mbalimbali”, alisema Rweikiza.
Aidha Rweikiza alisema mashindano haya mbali na kulenga kutoa burudani kwa wananchi na kunufaisha washiriki watakaojishindia zawadi pia yanalenga kukuza utalii, kutangaza utamaduni wa kitanzania na kutafanyika uhamasishaji wa tabia za afya zinazopewa kipaumbele katika makundi ya wavuvi na jamii inayowazunguka, ili kuepukana na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, Ugonjwa hatari wa Malaria, mimba zisiso tarajiwa, nk. hususani kwa vijana ambao wako katika hatari zaidi.
Sambamba na hayo, kutakuwa na promosheni za kinywaji cha Balimi Extra Lager katika maeneo mbali mbali.
Aliwataka wavuvi wengi wanaotaka kushiriki kuendelea kujiandikisha kushiriki kuanzia leo kupitia vituo 10 vya uandikishaji vilivyotengwa katika maeneo mbalimbali, Vilevile aliwataka wakazi wa jiji la Mwanza kujitokeza kwa wingi katika siku ya mashindano.
Naye Meneja Mauzo wa kampuni ya bia Tanzania (TBL) kanda ya Mwanza,Issa Makani,amesema kampuni imejitokeza kudhamini mashindano hayo mwaka huu kupitia kinywaji cha bia ya Balimi kwa kuwa imekuwa ikiyadhamini kwa zaidi ya miaka 10 na itandelea kuyadhamini kutokana na kuendelea kupata umaarufu mkubwa na kuleta burudani kwa wananchi sambamba na kuwaongeza kipato washiriki.