Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema sekta ya kilimo bado ina mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa kutokana na kuendelea kuchangia asilimia kubwa kwenye Pato la Taifa na kuajiri Watanzania wengi kuliko sekta zingine.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa ametoa kauli hiyo leo Desemba mosi, jijini Mwanza wakati akitangaza matokeo ya mwanzo ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyofanywa na NBS mwaka wa kilimo 2019/2020 matokeo.
Chuwa amesema utafiti uliofanyika umebaini kuwa sekta ya kilimo inachangia pato la taifa kwa wastani wa asilimia 27.5 na ndiyo chanzo kikuu cha ajira kwa kuajiri zaidi ya asilimia 65 ya nguvu kazi na chanzo kikuu cha fedha za kigeni kwa kuingiza wastani wa asilimia 24.7 ya fedha zitokanazo na uuzaji wa bidhaa za kilimo nje ya nchi.
Amesema matokeo ya sensa hiyo yameonyesha kuwa, kaya milioni 7.8 sawa na asimilia 65.3 ya kaya zote nchini, zinajihusisha na shughuli za Kilimo, kati ya hizo, kaya milioni 7.7 kutoka Tanzania Bara na 180,219 ni kutoka Zanzibar ambapo takriban asilimia 65 ya kaya hizo, zinajihusisha na shughuli za kilimo cha mazao tu, wakati asilimia 33 zinajihusisha na shughuli za kilimo cha mazao na mifugo, huku asilimia mbili zinajihusisha na shughuli za ufugaji tu.