Watu tisa wamefariki na wengine 180,000 kuathiriwa na kimbunga Gati kilichotokea nchini Somalia.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, inakadiriwa kuwa mifugo 7,500 ikiwemo ngaramia, kondoo na mbuzi pia imekufa kutokana na kimbunga hicho kilichosababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya Xaafuun, Karduush na Hurdiye.
Tathmini iliyofanywa na OCHA imeonyesha kuwa, kimbunga hicho pia kimeharibu karibu asilimia 75 ya majengo yanayomilikiwa na watu binafsi katika maeneo ya Xaafuun, Dardaare, Hurdiye na Karduush.
Pia shule, hospitali, ofisi za serikali na karibu asilimia 80 ya makazi ya watu zimeharibiwa na kimbunga hicho.