Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dr Festo Dugange amemhakikishia mbunge wa Muheza Khamis Mwinjuma al maarufu “Mwa FA” kuwa atashirikiana naye kusukuma maendeleo ya wanamuheza kufikia kiwango wanachokitarajia.
Dr. Dugange amesema kero na vikwazo wanavyovipata wanamuheza vitashughulikiwa kwa umuhimu unaostahili ili kuwahudumia wananchi wenye imani kubwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
‘Ikumbukwe kuwa hii ni miongoni mwa Wilaya kongwe na za kihistoria, ilikuwa eneo la kimkakati toka ukoloni na imebaki kuwa eneo muhimu kwa uchumi wa kati wa viwanda.
Tutahakikisha afya, elimu na miundombinu ya Wilayanya Muheza vinapewa kipaumbele ili kuwapa nafasi watu wake kuzalisha na kuchangia pato la Taifa kwa kiwango kinachofaa’ alisema Dr Dugange.
Awali katika ziara hiyo ya Naibu Waziri TAMISEMI wilani Muheza, “Mwana FA” mbunge wa jimbo la Muheza aliwasilisha kwa Dr Dugange kilio cha wanamuheza kwa kueleza mahitaji makubwa wa walimu, wataalam wa afya na hali isiyoridhisha ya miundombinu ya barabara katika jimbo na wilaya ya Muheza.
“Mwana FA” aliiomba OR TAMISEMI kuitazama kwa jicho la kipekee wilaya hiyo kutokana na historia , jiografia na mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa la Tanzania.
Dkt Dugange yupo mkoani Tanga akiendelea na ziara yake ya kukagua na kufuatilia utejelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa chini ya uratibu na usimamizi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI.