Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imelazimika kupunguza baadhi ya shamra shamra za maadhimisho ya kusherehekea miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ili kuokoa fedha na kuzielekeza katika matumizi mengine ya serikali,ikiwemo huduma za kijamii.
Dk. Mwinyi amesema hayo katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika leo katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini hapa.
Amesema Serikali ilikuwa na azma ya kuzipamba sherehe hizo kwa shamra shamra mbali mbali kama ilivyozoeleka na Wazanzibari wote, lakini kutokana na hali ya uchumi, sherehe hizo zimetekelezwa kwa njia tofauti na ilivyozoeleka.
Alieleza kuwa hali hiyo ni ya mpito na kubainisha kawa pale itakapotengemaa (katika siku za usoni), utaratibu wa kawaida wa maadhimisho ya sherehe hizo utarejea.
Alisema wakati umefika kwa Wazanzibari kujikita katika Uchumi wa Buluu, kwa kuzingatia shabaha ya Mapinduzi hayo ambayo ni kustawisha maisha ya wananchi wake.
Aidha, alisema Wazanzibari wanapaswa kupata huduma bora na stahili, ikiwemo elimu, afya na maji na kwa wale watakaohitaji kufanya biashara waweze kufanya shughuli zao bila kiuzuizi wala vikwazo vitokanavyo na rushwa.
Alisema Mapinduzi ya kiuchumi ndio mapinduzi yatakayotoa majibu ya changamoto ziliopo na vizazi vijavyo.
Alisema Wazanzibari wanahitaji Mapinduzi katika sheria na taasisi ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila bughudha wala vikwazo pamoja na kuwepo Mapinduzi katika Sanaa na Michezo ili kila mmoja aweze kutumia uwezo na kipaji chake kucheza na kujiendeleza kimaisha.
Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alisema Mapinduzi yanayohitajika yatawezekana endapo mambo tofauti yatatekelezwa, ikiwemo kuufungua Uchumi kwa kuweka mazingira mazuri .
Alisema ni azma ya serikali anayoiongoza kuvutia Wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendeleeza uchumi wa buluu.
Aidha, alisema eneo jengine linalohitaji Mapinduzi ni kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa kodi mbali mbali.
(@ikulu_habari)