Rais wa Marekani Donald Trump huenda akawa Rais wa kwanza kuondolewa madarakani siku chache kabla ya muda wake kumalizika baada ya Bunge la wawakilishi kupiga kura ya kumtoa madarakani, kura zilizopigwa ni 232 kwa 197 huku wajumbe 10 wa chama chake wakiunga mkono hoja ya kumuondoa.
Baada ya ya bunge la wawakilishi kupiga kura, hatma ya Rais huyo inabaki mikononi mwa Bunge la Senate ambalo nalo linatarajia kupiga kura kuidhinisha au kukataa maamuzi ya bunge la wawakilishi ya kumuondoa Rais Trump.
Bunge hilo linalodhibitiwa na wabunge wengi wa Democrat lilipiga kura siku ya Jumatano saa kadhaa baada ya mjadala mkali huku walinzi wa kitaifa wakiimarisha usalama ndani na nje ya jumba la bunge hilo
Trump ameingia katika historia ya kuwa Rais pekee ambaye amepigiwa kura ya kuondolewa madarakani mara mbili na bunge la wawakilishi, kufungiwa mitandao yake yote ya kijamii yote hiyo ikisababishwa na kauli zake zilizosababisha fujo za waandamanaji waliovamia jengo la bunge na kulishambulia.
Bwana Trump anaachia madaraka tarehe 20 mwezi Januari kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu mwezi Novemba uliomtangaza Joe Biden mshindi.
Shirika la kijasusi nchini Marekani FBI limeonya kwamba kuna uwezekano wa kuzuka kwa maandamano katika majimbo yote 50 kabla ya kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden wiki ijayo.