Chuo Cha Maji, kampasi ya Dar es Salaam kimefanya mahafali yake ya 12 katika Viunga vya Mlimani City Jijini Dar es Salaam, ambapo wanafunzi 529 wamehitimu huku miongoni mwao wakitunukiwa astashahada, stashahada na shahada ya kwanza.
Kwa upande wa shahada ni wahitimu 153, stashahada ni 355 na 21 kwa ngazi ya stashahada, kwa idadi yao 529 wanawake waliohitimu ni asilimia 32%.
Aidha katika mahafali haya mgeni rasmi alikuwa Waziri mwenye dhamana katika Wizara ya Maji Mh. Jumaa Aweso (Mb) ambaye pamoja naye aliambatana na Naibu wake Mh. MaryPrisca Mahundi (Mb) pamoja watendaji waandamizi wa wizara hiyo.
Pia Waziri Aweso wakati wa hotuba yake amegusia mchango adhimu unaotolewa na Chuo cha Maji pamoja na hamu thabiti ya Wizara ya Maji kufanya kazi na Chuo hicho katika kutatua changamoto za maji kwenye maeneo ya Mijini na Vijijni.
Zaidi Aweso amewamwagia sifa kedekede wahitimu hao kwa kusema kuwa wanaajirika huku akitaka Wizara ya Maji kuwatumia katika miradi mbalimbali, pamoja na kukabidhii miradi mitano kwa chuo hicho ili miradi hiyo kuwa ya mfano na ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa chuo hicho.
Waziri huyo ameitaja Wizara yake kuwa miongoni mwa Wizara zenye miradi lukuki kwa kubainisha kuwa hadi sasa Serikali ya Rais John Magufuli imetekeleza na kukamilisha miradi 1423, miradi 1268 ikiwa vijijini na 155 ikiwa maeneo ya mijini, miradi mingine zaidi ya 200 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji hivyo kuwataka wahitimu kuitazama miradi hiyo kama fursa ya kujiajiri kwa kuunda vikundi vya kusimamia na kuendesha miradi hiyo huku wakizikabili changamoto za maji mijini na vijijini.
Katika hatua nyingine Aweso amewataka wataalamu hao ambao wametunukiwa madaraja mbalimbali ya kitaaluma kuwa tayari kufanya kazi mahali popote nchini tena kwa kujitoa, kufanyakazi kwa bidii, uweledi, uadilifu na uaminifu wakati wanapozitatua changamoto zinazohusiana na maji kote nchini.