Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kwamba Washington DC inaingia kwenye hali ya dharura baada ya kuzuka vurugu katika jengo la bunge na kuleta wasiwasi kwa serikali juu ya kuwepo tatizo la usalama kwenye sherehe ya kuapishwa Rais mpya tarehe 20, mwezi huu.
Ikulu ya Marekani imetoa taarifa kuwa, hali hiyo itaendelea mpaka tarehe 24 na kuidhinisha wizara ya usalama na idara ya hatua za dharura kutumia vifaa na rasilimali zinazohitajika kuratibu na kusaidia kuweka usalama katika kipindi hicho.
Idara ya upelelezi ya Marekani imetoa onyo kuwa, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 20, miji mikuu ya majimbo 50 ya Marekani na mji wa Washington DC inaweza kukumbwa na maandamano yenye silaha. Bunge la Marekani na mabaraza ya serikali ya majimbo hayo yatakuwa maeneo lengwa ya kushambuliwa.