
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Prof. Kitila Mkumbo amezindua benki ya wajasiriamali wanawake inayo milikiwa na kikundi cha kikoba cha Women of Hope Alive.
Uzinduzi huo umefanyika jana Disemba 04,2021 katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, wakati wa kongamano la Mwanamke na Kikoba 2021 lililoandaliwa na kikundi hicho.
Wakati wa uzinduzi wa benki hiyo ijulikanayo kama ‘Women of Hope Alive Microfinance bank’, Prof. Mkumbo amesema kupitia benki hiyo wanawake wataweza kunufaika kwa kupata mikopo itakayosaidia kukuza vipato vyao na taifa kwa ujumla.
“Tunatambua katika tafiti kwamba wanawake wakifanikiwa katika biashara huwa 90% ya mapato yanainufaisha familia, na ukikopesha wanawake na wanaume, wanawake ni waaminifu zaidi hivyo basi benki kopesheni wanawake maana pesa zenu zitawahi kurudi”, amesema Prof. Mkumbo.
Kadhalika Prof. Mkumbo amekihakikishia kikundi hicho kuwa serikali itawaunga mkono katika utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake bila malipo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi hicho ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum (CCM) mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Mahawanga, amesema benki hiyo itakuwa ikitoa mikopo kwaajili ya wanawake wajasiriamali, ikiwa ni jitihada za kuiunga mkono serikali katika kuwainua wanawake kiuchumi.
“Benki ya Women of Hope Alive Microfinance itajikita zaidi katika kuweka na kutoa fedha pamoja na kutoa mikopo kwa wanawake wajasiriamali ndani na nje ya kikundi chetu na lengo ni kuiunga mkono serikali katika kumuinua mwanamke”, amesema Mahawanga.

Mahawanga ameongeza kuwa kikundi hicho kwasasa kitahakikisha kinawafikia wanawake wote katika jiji la Dar es Salaam lengo ikiwa ni kuwawezesha na kuwainua kiuchumi.
Kadhalika katika risala iliyosomwa na katibu wa kikundi, Saumu Mbwana, Benki ya WHA Microfinance itawafikia wanawake huku wakiamini kuwa benki hiyo itakuwa chachu ya maendeleo kwa wanawake nchini.
“Benki hii itakuwa msaada kwaakina mama, watapata mikopo na kulipa kodi kwaajili ya maendeleo ya nchi yetu” amesema Mbwana.
Kongamano hilo ambalo hufanyika kila mwaka na ni la tatu kwa mwaka huu, limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mary Masanja, Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi pamoja na mkuu wa wilaya ya Ubungo, Kheri James.