Watu wanane wamefariki, na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al Shabab kushambulia uwanja wa mkubwa wa ndege huko Mogadishu Somalia.
Msemaji wa polisi ameiambia BBC kuwa watano kati ya waliouawa ni raia wa kigeni akiwemo mwanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia- AMISOM. Wanamgambo wawili wa Al Shabab pia waliuawa katika shambulio hilo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Adde siku ya Jumatano.
Kwa mujnibu wa Msemaji wa polisi wa Somalia watu hao wanaoshukiwa pia kuwa wanachama wa kundi la al-Qaeda walijaribu kuvamia sehemu ya uwanja wa ndege wenye ulinzi mkali lakini walipigwa risasi na vikosi vya usalama waliokuwa wakifunga lango.
Uraia wa waliouawa bado haujatambuliwa. Sehemu iliyolengwa ya uwanja wa ndege ina kambi ya jeshi, ofisi za Umoja wa Mataifa na balozi kadhaa za kigeni.
Walioshuhudia tukio hilo wameiambia BBC kuwa walisikia milio mikubwa ya risasi na kushuhudia moshi mweusi ukifuka kutoka sehemu ya uwanja wa ndege.
Ripoti nyingine zinasema kuwa ofisi za Umoja wa Mataifa zilishambuliwa na makombora. Kundi hilo la wanamgambo katika siku za nyuma lililenga vituo vya serikali, vikosi vya usalama na raia na miezi ya hivi karibuni limeshuhudia ongezeko kubwa la mashambulizi katika mji mkuu na maeneo mengine ya nchi.
Haya yanajiri wakati ambapo Somalia inaendelea na uchaguzi wa bunge ambao umecheleweshwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.