Boti iliyokuwa imebeba wahamiaji kadhaa imepinduka katika bahari ya Mediterania nje ya pwani ya Libya jana Jumamosi, ambapo watu wasiopungua 19 wasiojulikana walipo wanadhaniwa kuwa wamekufa.
Kikosi cha ulinzi wa pwani cha Libya kimesema kundi la wahamiaji 23, raia wa Misri na Syria, waliondoka kutokea mji wa mashariki wa Tobruk mapema jana. Wahamiaji watatu waliokolewa na kupelekwa hospitali, na mwili mmoja umeopolewa huku juhudi za utafutaji zikiendelea.
Ajali hiyo ndiyo janga la karibuni zaidi la baharini linalowahusisha wahamiaji wanaojaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuingia Ulaya wakitokea taifa hilo la Afrika Kaskazini.
Libya imegeuka kituo kikuu cha usafirishaji wa wahamiaji wanaokimbia umaskini barani Afrika na Mashariki ya Kati, wakitumai kupata maisha bora barani Ulaya. Katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka 2022, wahamiaji wasiopungua 192 wamezamba baharini, na wengine wasiopuopungua 1,553 wanadhaniwa kuwa walifariki wakati wakijaribu kuja Ulaya mnamo mwaka 2021.