Iran imesema italipiza kisasi mauaji yoyote ya wanajeshi wake wanaouawa na Israel.
Shirika la habari ambalo halimilikiwi moja kwa moja na serikali la Tasnim limeripoti hayo leo kwa kumnukuu mkuu wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Hossein Salami.
Salami amesema hawatoshiriki tu kwenye mazishi ya mashahidi wao, bali pia watalipiza kisasi mara moja.
Salami ameonya kuwa huo ni ujumbe muhimu. Ameiambia Israel iwapo watarudia uovu wake, basi watashambuliwa kwa makombora ya Iran.
Walinzi wa Mapinduzi ya Iran walidai kuhusika na shambulizi la Machi 13 katika kile walichokiita ”vituo vya mkakati vya Israel” huko Erbil, mji mkuu wa jimbo linalojitawala la Wakurdi kaskazini mwa Iraq.
Shambulizi hilo lilionekana kama kisasi cha Iran baada ya Israel kuwaua wanajeshi wake nchini Syria, mshirika wa karibu wa Iran, katika shambulizi la anga la Machi 7.