Mshtakiwa huyo aliachiwa huru jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Yusto Luboroga, baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili.
Akisoma hukumu hiyo, alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 10 na mshtakiwa alijitetea mwenyewe.
Hakimu Luboroga alisema katika ushahidi uliotolewa na mashahidi hao, hakuna ushahidi ulioweza kumtia hatiani mshtakiwa, Mhasibu alipotoa ushahidi wake mahakamani alikana kuiba fedha hizo.
Mshtakiwa katika utetezi wake alidai kutoiba fedha hizo kwa kuwa yeye sio mweka saini na hakuwa na uwezo wa kuchukua fedha hizo, pia katika kipindi hicho hapakuwa na huduma ya fedha katika simu yaani simbanking.
Hakimu alisema mhasibu huyo pia alisema miamala yote iliyokuwa ikifanyika ilikuwa ikitumwa katika mfumo wa malipo na ilikuwa ikionekana na mahakama ilihitaji kuona nakala za miamala hiyo, lakini upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha.
“Hakuna ushahidi ulioonesha kwamba fedha zilipotea bali imeonekana mshtakiwa alichanganya miamala badala ya kuingiza kwa X ameingiza kwa Y, hivyo mahakama inaona mshtakiwa hakuiba,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo mahakama imeona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa na inamwachia huru.
Katika kesi hiyo mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na mashtaka 15, 14 kati hayo yakiwa ya kughushi miamala ya fedha na moja la wizi wa kiasi hicho cha fedha.
Katika shtaka la wizi ilidaiwa kwamba kati ya Januari hadi Septemba mwaka 2013 katika Kampuni ya SCI Tanzania Ltd, Upanga, Monica aliiba Sh. milioni 102 mali ya Kampuni hiyo zilizofika kwake kutokana na nafasi yake ya kuajiriwa.