Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelaani ukatili wa mauaji ya watoto na raia wengine wasioweza kujilinda huko Ukraine na kutoa wito wa kukomeshwa kwa mashambulizi kabla ya miji kugeuka kuwa makaburi.
Papa Francis ametoa rai hiyo wakati wa Ibada ya Jumapili katika uwanja wa St Peter mjini Roma, mbele ya waumini wapatao 25,000.
Amesema kwamba katika siku chache zilizopita mji wa Mariupol umegeuka kuwa mji wa mashahidi katika vita hiyo mbaya na kuongeza kwamba hakuna sababu za kimkakati zinazoweza kuhalalisha unyama, mauaji ya watoto, watu wasio na hatia na wale wasioweza kujilinda.
Francis pia amezishukuru nchi nyingi na wafanyakazi wa kujitolea ambao wanaendelea kuwasaidia wakimbizi kutoka Ukraine.