Mshambuliaji wa Yanga, Yacouba Songne anaweza kurejea uwanjani muda wowote kuanzia sasa baada ya kuwa nje kwa muda mrefu akitibiwa goti.
Yacouba aliumia katika mchezo dhidi ya Geita Gold Oktoba 2, mwaka jana ambao Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Jesus Moloko ambapo yeye alitoa pasi ya bao hilo.
Kauli hiyo imethibitishwa na daktari wa Yanga, Youssef Amar, amesema Yacouba kwa sasa yupo sawa na kuanzia Aprili Mosi ataanza mazoezi.
“Yacouba kwa sasa yupo salama na anaendelea vizuri tofauti na hapo awali ambapo hali ilikuwa mbaya zaidi, kwa sasa tunasubiri mpaka Aprili Mosi ndio aanze rasmi mazoezi ya ufiti ambayo ni pamoja na gym”amesema daktari Youssef Amar.
Aidha daktari huyo amesema baada ya hapo ataanza mazoezi na wenzake kwa ajili ya kujiandaa kucheza mechi za ushindani ambazo zitakuwa zimesalia msimu huu, tuna imani ataanza kupatikana mapema sana kwa kuwa maendeleo yake ni mazuri.