WAMILIKI wa hoteli kubwa za kitalii wamepewa muda wa siku saba kujiunga na mifumo ya kodi inayotumiwa na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ili kudhibiti ukwepaji kodi.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Sada Mkuya wakati alipokutana na wamiliki wa hoteli za kitalii kwa ajili ya kuona ukusanyaji wa mapato ya serikali unakwenda kwa mujibu wa sheria za kodi.
Alisema uchunguzi unaonesha baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wakiwemo wamiliki wa hoteli za kitalii hawajajiunga na mifuko ya ukusanyaji wa mapato ya serikali jambo ambalo halikubaliki kisheria.
Alisema serikali imeanzisha mifumo hiyo na kuitungia sheria za kodi kwa lengo la kuona kodi zinakusanywa ipasavyo na zinatumika vizuri.
‘’Wamiliki wa hoteli za kitalii natoa muda wa siku saba kuhakikisha mnatumia mifumo ya kulipa kodi kwa mujibu wa sheria hatua ambayo itasaidia serikali kupata kodi zake sahihi,” alisema.
Aidha, Mkuya aliwataka watumishi wa Bodi ya Mapato Zanzibar kufanya ukaguzi wa kodi kwenye hoteli za kitalii ili kudhibiti wamiliki wanaokiuka sheria za ukusanyaji wa kodi. ‘’Kazi ya ukaguzi kwa wafanyabiashara na wamiliki wa mahoteli nataka muifanye mara kwa mara kwa sababu wapo wanaokwepa kodi na kufanya ujanja,’’ alisema.
Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar, Yussuf Mwenda alisema wamejipanga kuhakikisha wanakusanya kodi ipasavyo na kuziba mianya yote iliyokuwa ikivujisha mapato.
Alisema wameanza kuwakagua wafanyabiashara wote kuona kama wanatumia mfumo unaokubalika wa kufanya malipo ya serikali kwa mujibu wa sheria.
Meneja wa hoteli ya kitalii ya Malindi, Mohamed Ismail alisema wapo tayari kutumia mifumo halali ya kodi inayotumika kwa malipo ya serikali.