Baadhi ya Wananchi wamefunga barabara baada ya John Frank (7) mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Nguzombili iliyopo halmashauri ya mji Geita, kugongwa na roli la mchanga aina ya ISUZU T177 AHH.
Mwanafunzi huyo amegongwa wakati akivuka barabara hali iliyopelekea wananchi kufunga barabara hiyo mpaka serikali itakapochukua hatua za tahadhari kutokana na eneo hilo kuambatana na shule mbili zenye wanafunzi Zaidi ya 8000.
Baadhi ya wananchi wenye majonzi na hasira kali wanasema katika eneo hilo watoto wamekuwa wakigongwa mara kwa mara hivyo wameiomba serikali kulipatia uzito ili kulinda maisha ya watoto wao.
Diwani wa kata hiyo Dotto Zanzui amesema baada ya ajali hiyo RTO amesema kuwa anatoa askari wa usalama barabarani ili wawe wanasaidia kuwavusha watoto katika barabara hiyo.
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Geita Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kifo cha mwanafunzi huyo huku akisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari hilo kwani eneo hilo linajulikana na kwamba dereva ni mkazi wa eneo hilo pia.