Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Daniel Chongolo amesema wakati huu Chama hicho kikiwa kwenye Mchakato wa Uchaguzi wa Ndani, kimetoa fursa na haki sawa ya Kuchagua na Kuchaguliwa, hivyo ni aibu kuona baadhi ya Wasimamizi kuamua kwa maslahi yao Binafsi Kuiminya haki hiyo isiwafikie Wana CCM.
Kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu huyo wa CCM, amepiga marufuku Urasimu huo akitaka Makatibu wa Matawi wa Chama hicho kutowanyima fomu za Kugombea nafasi mbalimbali kwenye Chama hicho kwa ajili ya Kulinda maslahi yao Binafsi.
Chongolo ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa Ziara yake iliyolenga kuzungumza na halmashauri kuu za Wilaya ya Ubungo na Kinondoni.
“Ninawaagiza Makatibu wa wilaya zote nchini, maeneo yote ambayo tumebaini yana changamoto ya watu kunyimwa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, tunarudisha zoezi la kutoa fomu, tunataka wale wote wenye dhamira ya kuchukua fomu wachukue bila kuwekewa vizuizi, hiki sio chama cha mtu, hiki sio chama cha maslahi binafsi, hiki chama ni cha wanachama, na ni lazima tutende haki kwa kuwa katiba yetu ya CCM inatutaka tufanye hivyo” amesisitiza Chongolo.
Pia amesema kwenye maeneo kadhaa ikiwemo Ubungo, Babati, Mbeya na Tabora, Chama hicho kimebaini baadhi ya watu wamechukua kadi ili kuwapa watu ambao watatumika kuwapigia kura.
“Ninatoa agizo kwa makatibu wa wilaya Nchini, vitabu vilivyokuwa vimehakikiwa ndio vitumike kwenye kupiga kura na sio vinginevyo, tutafuatilia na tukibaini kuna maeneo ambapo vitabu vilivyokuwa vimehakikiwa vimeongezwa majina wakurugenzi (Makatibu) wa uchaguzi watawajibika, hili sihitaji kusisitiza tutakutana baadae na hili ni kwa ngazi zote” ameongeza Chongolo.