ADVERTISEMENT
Ameandika GIFT MACHA
Aishi Manula. Inavutia sana kulitamka jina lake. Limekaa kipekee kama ilivyo kwa uwezo wake uwanjani.
Ni golikipa mmoja wa kisasa kuwahi kutokea nchini. Nafurahi zaidi kumtazama akiwa golini. Sina wasiwasi pindi anapokaa langoni. Iwe Simba ama Taifa Stars. Hapa nchini kwa sasa kuna Manula halafu ndio makipa wengine. Yaani magolikipa wengine karibu wote nchini wanatamani kuwa kama Aishi Manula.
–
Hata mkongwe Juma Kaseja anafurahi kuona anaondoka lakini ameiacha Tanzania kwenye mikono salama ya Manula. Yes, kwa Tanzania Kaseja ndiye kipa bora zaidi katika karne hii ya 21. Katika ubora wake ilikuwa ni jambo gumu sana kuziona nyavu mbele yake.. Angepaa kwenda popote kulinda lango lake..
–
Watu walikuwa na hofu kuwa baada ya Kaseja angekuja nani? Ni kweli kina Deo Munishi, Ally Mustapha na wengineo walifanya vizuri, lakini hawakufika kwenye kilele alichokuwa Kaseja.. Lakini Manula amefika. Tena mapema sana. Uzuri wa Manula ni kwamba amepunguza sana makosa aliyokuwa nayo kipindi cha nyuma. Pamoja na uwezo mkubwa aliokuwa nao, bado kuna nyakati alifungwa magoli mepesi.. Lakini siku hizi huwezi kuliona tena hilo. Ameimarika vilivyo.

Tazama mechi za CAF ambazo Simba ilicheza msimu huu.. Manula alikuwa nyota wa mchezo karibu mechi zote za ugenini. Alijua kuwakera wapinzani wa Simba. Angepangua hata mashuti ambayo kila mtu alidhani ni goli. Pili amekuwa imara zaidi kwenye mikwaju ya penalti. Siyo msimu huu tu, kila msimu Manula ni shujaa katika eneo hilo. Majuzi nilikuwa na uhakika kuwa hawezi kufungwa penalti zote tano na Orlando Pirates, na kweli alicheza moja..
.
Wakati huu ambao Manula anafanya vizuri, ni vyema tukampa pongezi zake. Ni nadra sana golikipa kuwa kwenye kiwango bora kwa miaka sita mfululizo kama ambayo imekuwa kwa Manula.. Tena uzuri ni kwamba siku zinavyosonga ndio anakuwa bora zaidi. Ukweli mchungu ni kwamba hata Yanga inatamani kuwa na Manula. Ni golikipa anayemvutia kila mtu.
ADVERTISEMENT