Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitia barua kwa umma jana Jumamosi Aprili 16, 2022, umelaani vikali kitendo cha kinyama kama kinavyoonekana katika video inayosambaa mitandaoni kilichofanywa na baadhi ya Askari Mgambo wa Halmashauri, kuchukua bidhaa aina ya ndizi za Wajasiriamali wadogo yaani Machinga.
Bidhaa hizo zilizokuwa zinauzwa katika toroli na zinaonekana kutupiwa katika gari ya Halmashauri na Mgambo hao kinyume na taratibu za Oparesheni ya kuwaondoa Machinga katika maeneo yasiyo rasmi tukio ambalo ni la unyanyasaji na linahatarisha usalama wa mali za Wafanyabiashara ikiwemo kupoteza ubora na kuharibika kabisa.
Halmashauri ya Jiji la mwanza haihusiki kwa namna moja au nyingine kuagiza Askari kuendesha zoezi hili kwa namna linavyoonekana bali ni utashi na nía ovu ya Askari Mgambo hao jambo mbalo ni kinyume kabisa cha maelekezo ya oparesheni.
Kufuatia hili Uongozi wa Halmashauri umechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha Askari Mgambo waliohusika kutojihusisha katika Oparesheni ya kuwaondoa machinga katika maeneo yasiyo rasmi wakati taratibu nyingine za kisheria zikiendelea kufanyika dhidi ya wahusika wote.
Halmashauri inaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa umma hasa wafanyabishara waliopata kadhia hii na kusisitiza kuwa Halmashauri inaongozwa kwa miongozo, sheria na taratibu kwa kuzingatia utu na maadili na inatoa wito kwa Askari Mgambo kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia miongozo, sheria na taratibu.