Iran imeanzisha tena mazungumzo na hasimu wake wa kikanda Saudi Arabia, baada ya kusitishwa kwa mazungumzo ya siri mjini Baghdad miezi kadhaa iliyopita.
Tovuti ya habari ya Irani ya Nour, inayotajwa kuwa karibu na Baraza la Juu la Usalama la Taifa, imesema awamu ya tano ya mazungumzo ilifanyika Baghdad na kuhusisha maafisa usalama kutoka pande zote mbili pamoja na maafisa kutoka Iraq na Oman.
Iran, nchi kubwa zaidi ya Waislamu wa Shia na Saudi Arabia, ambayo ndiyo taifa kubwa zaidi la madhehebu ya Sunni, zilivunja uhusiano wa kidiplomasia mnamo 2016, baada ya taifa hilo kumuua aliekuwa mhubiri mashuhuri wa kishia Nimr al-Nimr.
Hatua hiyo ilizusha maandamano miongoni mwa Wairan wenye hasira wakipinga kunyongwa kwa mhubiri huyo na kuvamia balozi mbili za Saudia huko Iran, hatua iliochochea uhasama wa miaka mingi kati ya mataifa hayo.
Mnamo Machi, Tehran ilisema ilisimamisha kwa muda mazungumzo hayo, yaliyolenga kutuliza mvutano wa miaka mingi, baada ya Saudi Arabia kuwaua watu 81 waliopatikana na hatia ya mauaji na kujihusisha na makundi ya wanamgambo.