Mshambuliaji kinda wa Kimataifa wa Tanzania, Kelvin John amezidi kuweka historia katika Soka la kulipwa barani ulaya, baada ya Jana kutwaa Ubingwa wa Ligi kuu ya Vijana chini ya umri wa miaka 21 nchini Ubelgiji kwa msimu wa 2021/22.
Kelvin John alifunga goli moja na kuisaidia klabu yake KRC Genk U21 kupata ushindi wa goli 2-1 dhidi ya Royal Charleroi U21 kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Neuville,ulioko katika manispaa ya Montignies-sur-Sambre Mkoa wa Hainaut nchini Ubelgiji.
Genk U21 wametwaa ubingwa huo baada ya kufikisha alama 52 ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote kwenye Ligi hiyo. Katika michezo 19 waliocheza wameshinda michezo 17 na kutoka sare michezo miwili wakiwa na michezo mitatu mikononi huku kufunga jumla ya mabao 61 na kuruhusu kufungwa mabao 17.