Mtoto Salah Jackson (5) mwenye ulemavu wa viungo, mkazi wa kijiji cha Makiwaru, mkoani Kilimanjaro amefariki dunia kutokana na njaa na kisha mama yake mzazi kumzika kimya kimya usiku wa manane.
Mtoto huyo anadaiwa kuzikwa na mama yake mzazi aitwaye Rebecca Siowi (30) usiku wa kuamkia Aprili 22, 2022 nyumbani kwa bibi yake walikokuwa wakiishi yeye pamoja na mama yake baada ya mume kumtelekeza na watoto watano.
Tukio hilo liligundulika baada ya mtoto huyo kutoonekana jioni ya Aprili 21 nyumbani alikokuwa akiishi kwa bibi yake, ambapo bibi yake huyo alifanya jitihada za kumtafuta mjukuu wake huyo bila mafanikio ndipo Aprili 22 alipobainika kuwa amezikwa.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amekiri kuwepo kwa tukio hilo, akisema baada ya kupata taarifa hiyo kutoka kwa wananchi walifika eneo la tukio kuona sehemu alipozikwa mtoto huyo.