Marekani imetoa agizo kwa raia wake wasiokuwa wafanyakazi wa dharura katika ubalozi wake mdogo mjini Shanghai, waondoke. Mji huo wa China umewekwa chini ya sheria kali za kudhiti kuenea virusi vya Corona,ambapo shughuli za kimaisha zimefungwa.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema amri iliyotangazwa jana Jumatatu usiku inawalenga wafanyakazi wake wa ubalozi mdogo wasiokuwa na majukumu ya lazima na inatofautiana na tangazo la wiki iliyopita la kuwataka wamarekani waondoke Shanghai kwa khiyari yao.
Wakaazi wengi wa mji huo wenye idadi ya watu milioni 26 wamefungiwa majumbani mwao kwa kipindi cha hadi wiki tatu. China imechukua hatua hiyo kuendeleza mkakati wake wa kudhibiti kikamilifu ugonjwa wa Covid-19 na kuzuia mripuko wa kusambaa virusi vya ugonjwa huo kwa kuwatenga na kuwapima watu kwa wingi.