Mwanamuziki na mjasiriamali, Zena Yusuf Mohammed maarufu nchini Shilole, leo Aprili 20, 2022 ni siku anayotimiza mwaka mmoja tangu alipofunga ndoa na mumewe Rommy3D.
Wawili hao kwa pamoja wametumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kutumiana jumbe za upendo kama sehemu ya kusherehekea mwaka mmoja wa ndoa yao.
Huku Shilole akienda mbali zaidi kiasi cha kudokeza kuhusu historia fupi ya penzi lao, wakati waliokutana, kuachana na kurudiana tena mapaka hatma ya kufikia uamuzi wa kuwa wanandoa.
“Nilimfahamu Rajabu miaka mingi kidogo iliyopita. Maisha yana siri zake na mapito yake, tukapita pamoja tukatengana halafu kudra za Mungu zikaturudisha pamoja tena kama miaka miwili iliyopita.
Mungu ndiye muandishi wa hadithi za maisha yetu, yeye mwenyewe anajua kwa nini tulitengana na kwa nini nilipitia yote niliyopitia kabla ya kukutana tena na mume wangu.
Ninachojua mimi, kukutana tena na Rommy na kufunga naye ndoa ni zawadi kubwa zaidi niliyokirimiwa na Allah.
Ndoa hii ndio nilichotaka, Mume huyu ndiye niliyestahili, hata wakati ule ‘mnabet’ kuwa ndoa itadumu mwezi mmoja na mimi nilimuachia Mungu aamue hatma yetu kwa rekhma zake.
Tuko hapa kwa uwezo wa Mungu na yeye Inshaalah ataendelea kulinda ndoa yetu.
Tunamshukuru Mungu leo tunapotimiza mwaka mmoja wa ndoa yetu. Namshukuru Mume wangu kwa kuendelea kuwa mume bora kwangu na kiungo muhimu cha furaha kwetu. nakupenda sana Mume wangu” ameandika Shilole.
Kwa upande wa mume wa Shilole Rommy 3D yeye ameweka wazi mambo kadhaa kuhusu magumu waliyoyapitia na namna walivyojikita katika kutimiza lengo la wao kuingia kwenye ndoa bila kusikiliza maneno ya watu ambao kundi kubwa lilikuwa likitabiri kuwa pengine wawili hao hawatafika popote.