Mwanamke wa Kijapani ambaye aliidhinishwa kuwa na umri mkubwa kuliko wote duniani, amefariki akiwa na miaka 119. Kane Tanaka alizaliwa Januari 2, 1903, katika mji wa Fukuoka ulio kusini magharibi mwa Japan, mwaka huohuo ndugu wawili wa familia ya Wright walirusha ndege huku Marie Curie akishinda tuzo ya Nobel.
Tanaka alikuwa katika hali nzuri kiafya hadi hivi karibuni na aliishi katika nyumba ambayo alikuwa akipata matibabu na alipenda michezo, kutafuta majibu ya hisabati, kunywa soda na kula chocolate.
Enzi za ujana, Tanaka aliendesha biashara tofauti, ikiwemo ya kuuza sindano na keki. Alioana na Hideo Tanaka karne moja iliyopita, mwaka 1922, akizaa watoto wanne na kuasili wa tano.
Alikuwa amepanga kutumia kiti cha magurudumu ili kushiriki mbio za mwenge wa Olimpiki wakati wa Michezo ya Tokyo mwaka 2021, lakini janga la corona lilimzuia.
Wakati taasisi ya Guinness World Records ilipomthibitisha kuwa ndiye mwanamke mwenye umri mkubwa aliye hai mwaka 2019, aliulizwa ni wakati gani ulikuwa wa furaha sana kwake, alijibu “sasa”.
Shughuli zake za kila siku zilielezewa wakati huo kuwa ni kuamka saa 12:00 asubuhi na kutumia mchana kusoma hesabu na kufanya mazoezi ya kuandika herufi. Gavana wa eneo alilokuwa akiishi, Seitaro Hattori alimwagia sifa Tanaka baada ya kufariki Aprili 19.