Mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Kenya Joyce Chepkirui (33) amefungiwa kwa miaka 4 kushiriki katika mchezo huo kutokana na utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu (doping).
Mwanariadha huyo alishinda mbio za mita 10,000 katika mashindano ya Common Wealth Jijini Glasgow mwaka 2014 na mwaka huohuo aliongoza mbio za urefu wa mita 10,000 kwa upande wa Afrika katika Mashindano yaliyofanyika Marrakech nchini Morocco.
Chepkirui alisimamishwa kuanzia mwaka 2019 baada ya wataalamu kugundua utofauti katika vipimo vya damu vilivyofanyika kati ya mwaka 2016 na 2017.
Matokeo yote ya mwanariadha huyo kati ya Aprili 2016 na Agosti 2017 ambayo yanajumuisha nafasi ya tatu aliyoshinda Jijini Boston, Marekani yatafutwa na atapoteza medali na tuzo zote alizopokea katika kipindi hiko.
Kwa muda sasa wakala wa Kimataifa wa kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu, iliiweka Kenya kwenye kundi la nchi zenye hatari kubwa ya matumizi ya dawa hizo.
Wanamichezo kutoka Kenya hutakiwa kupitia vipimo mara 3 ndani ya miezi 10 kabla ya kwenda kushiriki mashindano ya Kimataifa ikiwemo Olimpiki