Kocha wa klabu ya Yanga SC, Nasreddine Nabi ataukosa mchezo dhidi ya watani zao Simba SC , kutokana na adhabu aliyopewa na kamati ya mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Nabi ataikosa dabi hiyo, itakayopigwa Aprili 30, 2022 uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya kupewa kadi nyekundu dhidi ya Geita Gold, mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) iliyochezwa Aprili 10.
TFF imemhukumu Nabi kwa kosa la kuwashambulia kwa lugha matusi waamuzi wakati wanatimiza majukumu yao, hivyo adhabu hiyo itapelekea kutoruhusiwa kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo sambamba na eneo la linapokaa benchi la ufundi la timu yake. Mbali na adhabu hiyo, pia atakosa michezo mitatu sambamba na kutakiwa kulipa faini ya sh 500,000.